Balozi wa Mji Wangu wa Kuasili
Kipindi Kazini nchini Japani kinaangazia maisha ya raia wa kigeni wafanyao kazi nchini humo. Wakati huu, tunamtembelea Anika Godek raia wa Poland katika manispaa ya mji wa Fuchu jijini Tokyo anakofanya kazi ya kunadi uzuri wa mji huo kwa watalii wa kigeni.
Anika Godek amekuwa akifanya kazi kama afisa uhusiano wa umma kwenye manispaa ya mji wa Fuchu tangu 2018.
Kazi ya Anika hasa ni kuzunguka mjini Fuchu, akizuru maeneo mbalimbali na kuripoti matukio kwa kuandika makala kwenye tovuti ya mji na mitandao ya kijamii kwa ajili ya hadhira duniani kote.
Tangu Anika alipoanza kunadi mji huo, akaunti za mitandao ya kijamii za Fuchu zimekuwa maarufu.
Anika anamtembelea Kikuchi, mkulima wa matunda ya blueberry mjini Fuchu. Majaribio ya kwanza ya kilimo cha biashara cha blueberry nchini Japani yalifanyika Fuchu miaka ya 1960. Sasa eneo hilo lina mashamba mengi ya blueberry.