Kuishi na Dubu
Tunamtembelea msichana kutoka Uingereza ambaye amekuwa akifanya utafiti na ulindaji wa dubu pori weusi wa Asia nchini Japani. Kazini nchini Japani - kipindi kinachoangazia maisha ya watu kutoka duniani kote waliyoichagua Japani kuwa sehemu yao ya kazi.
Amelia Joyce Hiorns ana umri wa miaka 24. Kazi yake ni kutafiti na kuwalinda dubu pori huko Karuizawa, mkoani Nagano.
Amelia amekuwa akifanya kazi na shirika lisilo la kujipatia faida lijulikanalo kama Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori cha Picchio tangu mwaka 2019. Kituo hicho kimepewa jukumu na serikali ya eneo kutafiti hali ya maisha ya dubu.
Usiku wa manane, Amelia na mfanyakazi mwenziwe wanawasaka dubu waliowekewa kola kwa kutumia kifaa cha kunasa mawimbi kama sehemu ya doria ya usiku. Kwa sasa kituo hicho kinafuatilia mienendo ya dubu karibu 40.
Kuna mbwa dubu wawili kituoni hapo. "Mbwa dubu" hao wamepata mafunzo yanayowawezesha kuwatambua dubu kwa harufu na kuwafukuza hadi misituni.