Nguvu ya Kumbukumbu
Katika kipindi hiki, tumetembelea kituo cha kuwahudumia wazee katika mkoa wa magharibi mwa Japani wa Kochi. Watumiaji wengi wa kituo hiki wanasumbuliwa na ugonjwa wa kupoteza fahamu, yaani dimentia, hivyo walianzisha mradi wa kupunguza kasi ya hali ya ugonjwa kadiri iwezekanavyo. Wanatumia njia ya kufanya nao mahojiano mtandaoni. Tutafuatilia jitihada za kituo hiki katika kutunza rekodi za kumbukumbu za watumiaji wake.
Kufuatia kuenea kwa virusi vya korona, Choro Daigaku, ama "chuo kikuu cha wazee" kilianza kuendesha mahojiano ya "kiki-gaki" au "kusikiliza na kuandika" kupitia njia ya mtandao.
Watu wengi kote nchini walijitolea kama wahudumu kituo hicho kilipoamua kuajiri wafanyakazi wapya hasa ili kusimamia usikilizaji na uandishi.
Kido Hisae, ni mwandishi wa habari wa kujitegemea anayeangazia tajiriba za wakati wa vita, anashiriki mradi huo akitumai kusaidia kutunza rekodi za tajiriba za watu wengi kadiri iwezekanavyo.