Fuata Moyo Wako: Mtengeneza Bustani Mwenye Nywele za Kijani
Aoki Mariko ni mtengenezaji bustani kijana kutoka mjini Nagai, mkoani Yamagata kaskazini mashariki mwa Japani. Bustani zake zinabainisha sifa ya mmiliki wake zikiwa na maua mbalimbali ya msimu na sehemu ya kupumzikia. Anawezaje kutengeneza bustani kama hiyo? Tunaungana naye katika maisha yake ya kila siku ya utengenezaji bustani ambazo watu wanaweza kuishi na kuzifurahia.
Aoki Mariko alianza kuwa maarufu mwaka 2018, aliposhinda tuzo kubwa katika moja ya mashindano makubwa ya maswala ya bustani nchini Japani. Anapata maombi karibu 10 kwa mwaka ya kutengeneza bustani.
Katika muda wake wa ziada, anajaribu vitu vingi kwenye bustani yake bila kuchoka. Anachunguza vitu kama namna mimea inavyoeneza mizizi yake au namna anavyoweza kukuza uimara wa mimeo hiyo. Amepanda miche zaidi ya 1,000 hapo.
Bustani zake zinajulikana kwa kuhitaji utunzaji mdogo. Siri ni uchaguzi wa mimea. Anayoichagua ni mimea ya kudumu. Siyo tu kwamba inavutia hasa yenyewe, bali pia inachanua maua kila mwaka bila kusaidiwa na mtu.