Maombi ya Amani kutoka Okinawa kuelekea Ukraine
Tunayemuangazia katika kipindi hiki ni Katarin Honma, raia wa Ukraine anayeishi mkoani Okinawa. Wakati akifanya kazi kama mhandisi, alifurahia maisha matulivu mkoani humo, akioka mikate kwa kutumia karoti zinazolimwa Okinawa, hadi pale uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulipobadilisha maisha yake ya kila siku. Hii ni simulizi inayounganisha Ukraine na Okinawa, makazi mawili ya Katarin. (Kipindi hiki kilitangazwa Juni 7, 2022.)
Katarin anatokea Odesa, mji wa bandari uliopo kusini mwa Ukraine. Alikuja Japani 1992 na kwa sasa anaishi mjini Itoman kwenye kisiwa cha Okinawa.
Katarin anaoka mikate ya karoti jikoni mwake kila siku. Anatumia karoti zinazolimwa mjini Itoman ambazo umbo lake limeharibika na kwa kawaida huwa zinatupwa.
Alipobaini uvamizi wa Urusi, Katarin aliendelea kuwapigia simu marafiki zake kuthibitisha ikiwa walikuwa salama.
Akihofia hali ya Katarin, Eimori Mitsuru (kushoto) alimpeleka Katarin mahali ambako wakazi wa Okinawa walioshuhudia athari za vita huombea kuwepo kwa amani duniani.