Kutengeneza Bia Inayoendana na Kyoto
Mji mkuu wa zamani wa Japani, Kyoto unajivunia uzuri wa utamaduni wa muda mrefu wa nchi hiyo. Mjini humo kuna kiwanda cha bia kilichofunguliwa na raia watatu wa kigeni wanaoipenda Kyoto. Biashara ilistawi mwanzoni ila janga la korona likaivuruga. Kipindi hiki kinawafuatilia watatu hao katika juhudi zao za kuendeleza sera yao ya kutengeneza bia yenye asili ya Kyoto, hata katika nyakati ngumu. (Kipindi hiki kilitangazwa Januari 11, 2022.)
Chris Hainge kutoka Marekani alifundisha Kiingereza katika shule moja mkoani Aomori kabla ya kufanikisha ndoto yake ya kuhamia Kyoto. Mwaka 2015, alifungua kiwanda cha bia pamoja na marafiki zake.
Kiwanda cha bia kimejizolea umaarufu kutokana na ladha yake tamu na harufu nzuri ya asili, lakini kwa sababu sheria za kukabiliana na korona ziliwekwa kwa wateja wa baa na migahawa, manunuzi yalipungua kwa hadi asilimia 97.
Watatu hao wamenuia kutengeneza bia ya asili ya Kyoto kwa kutumia mihopi ya eneo hilo.
Wakihangaika kustawi wakati wa janga, wamefanikiwa kutengeneza bia kwa kutumia mihopi inayolimwa mjini Yosano kaskazini mwa mkoa wa Kyoto.