Pamoja Tunaweza Kujikwamua!
Tunamwangazia mzawa wa Vietnamu Do Van Tuan, mwenyekiti wa Chama cha Wavietnamu Sendai, anayewasaidia Wavietnamu wenziwe wenye shida mbalimbali. Janga la virusi vya korona limewaathiri raia wa kigeni wanaoishi Japani; wengi wakipoteza ajira, wengine wakikosa hata pahali pa kuishi. Tangu wakati wa hali ya dharura, Tuan amepokea maombi mengi ya msaada kuliko ilivyowahi kutokea awali. (Kipindi hiki kilitangazwa Novemba 10, 2020.)
Do Van Tuan anawasilisha chakula na mahitaji mengine Wavietnamu wenziwe wenye uhitaji.
Tangu hali ya dharura ilipotangazwa, Tuan amekuwa akihifadhi vyakula alivyonunua mwenyewe na kuviwasilisha kwa wanaohitaji wakati wowote.
Tuan alikuja Japani akitokea Vietnamu miaka minane iliyopita. Amejenga taaluma yake akifanya kazi kama mkalimani, mfasiri na mwalimu wa lugha.
Wavietnamu hujifunza Kijapani kutoka kwa walimu Wajapani wanaojitolea katika darasa lililoanzishwa na Tuan. Wakitiwa huruma na kazi ya Tuan, Wajapani wengi wanaungana naye.