Kukaa Salama Kwenye Theluji
Japani ni mojawapo ya nchi duniani ambazo theluji nyingi hudondoka. Kudondoka kwa theluji ni jambo la kawaida hata katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu, mara kwa mara kusababisha majeraha kwa watu na ajali za barabarani. Hebu tujifunze unachoweza kufanya ili kukaa salama kutokana na theluji katika maeneo ya mijini. (Kipindi hiki kilitangazwa Machi 1, 2023.)
Mwanahabari wetu Chairat Thomya (kushoto) anatembelea Kituo cha Utafiti wa Theluji na Barafu kufanya mahojiano na Nakamura Kazuki, mkurugenzi wa kituo hicho na mtaalam wa majanga ya theluji (kulia).
Kituo hiki cha utafiti ni mojawapo ya vituo vichache duniani vinavyoweza kutengeneza theluji inayofanana sana na theluji asilia.
Kuna mambo matatu ya kuangalia wakati theluji inapodondoka: barabara za barafu zinazoteleza; dhoruba za theluji; na theluji inayodondoka kutoka juu ya paa.
Katika jaribio la kutumia kifaa kinachoweza kuigiza dhoruba ya theluji, Chairat anapata tajiriba ya kimbunga chenye upepo wa kasi ya mita 5 kwa sekunde na kupata ugumu wa kuacha macho yake wazi pamoja na kutoweza kuona vizuri.