Tahadhari ya Moto Wakati wa Msimu wa Baridi
Japani imeshuhudia kutokea mara kwa mara kwa moto wakati wa msimu wa baridi kutokana na hewa kavu na ongezeko la matumizi ya vifaa vya kutoa joto. Tunashirikishana na wasikilizaji wetu vidokezo vya jinsi ya kujikinga na moto na nini cha kufanya pale unapotokea. (Kipindi hiki kilitangazwa Februari 1, 2023.)
Mwanahabari wetu Janni Olsson anatembelea Kituo cha Mafunzo ya Usalama wa Maisha cha Ikebukuro kilichopo jijini Tokyo, kinachotoa mafunzo ya kuigiza majanga mbalimbali. Mkurugenzi wa kituo hicho, Harashige Yoshiro, aliyewahi kuwa mzimamoto anamwelekeza.
Janni anapata tajiriba ya kwanza ya kupambana na moto unaowaka kwa msaada wa kifaa cha kuigiza na anajifunza jinsi ya kutumia kifaa cha kuzimia moto.
Nchini Japani, unapiga simu namba 119 kuita gari la zimamoto. Hata kama huna ustadi wa lugha ya Kijapani, huduma zinapatikana kwa lugha mbalimbali ikiwemo Kiingereza na Kichina.
Sio tu miale ya moto inayoweza kuua wakati wa moto bali pia moshi. Kituo hiki kinatoa mazoezi ya kujiokoa kwa dharura kwa kutumia moshi usio na madhara. Hakikisha unafunika pua na mdomo wako na vifaa kama vile leso na tembea kwa kuchutama wakati wote wa kujiokoa ili usivute moshi.