Kushughulikia Mahitaji ya Wanawake Katika Majanga
Kukaa katika makazi ya dharura baada ya janga kwa kawaida kunaweza kuhusisha ugumu hususani kwa wanawake. Ni maandalizi gani ya kimwili na kiakili ambayo wanawake wanatakiwa kuyafanya wakati wa dharura? Tulimuuliza Ohuchi Yukiko, kiongozi wa usimamizi wa majanga katika mji wa Sendai, ambaye kwa kawaida alikaa katika makazi ya muda baada ya Tetemeko Kuu la Japani Mashariki mwaka 2011.
Ohuchi alimuonyesha Kate J, begi lake la mgongoni wakati wa kuhama, lenye vifaa vya dharura vya chooni, mablanketi ya alumini, vifaa vya usafi wakati wa hedhi, losheni pamoja na bidhaa zingine za kutunza ngozi anazozipenda. Kuweka vitu unavyoviona muhimu katika begi siyo jambo la gharama.
Miongoni mwa vitu katika begi la mgongoni ni chupa ya plastiki yenye matundu. Unapoifungua chupa ya plastiki yenye maji, inaweza kutumika kama bomba la maji kwa ajili ya kujisafisha chooni.
Mji wa Sendai umeandaa mwongozo wa usimamizi wa majanga, kulingana na uzoefu wake katika janga la mwaka 2011. Unahusisha taarifa mbalimbali za kuhakikisha kuwa wanawake wanaweza kukaa katika makazi ya muda katika hali ya usalama, ikiwemo kujenga chumba cha kunyonyeshea ambacho kinaweza kufungwa au kuandaa sehemu tofauti kwa wanaume na wanawake ya kutundika nguo.
Ohuchi amesomea utayari wa majanga na kupata mafunzo. Kwa sasa ameelekeza juhudi zake katika kuendeleza viongozi wanawake katika usimamizi wa majanga ambao watafuata nyayo zake.