Milipuko ya Volkano
Japani ni moja ya nchi zilizo na volkano nyingi zaidi duniani. Mji wake mkuu wa Tokyo, upo karibu na Mlima Fuji, ambao ni volkano hai inayoweza kulipuka muda wowote. Katika kipindi hiki, tutajifunza kutoka kwa mtaalam kinachoweza kutokea katika mlipuko wa volkano na jinsi ya kujilinda wakati wa dharura kama hiyo.
Japani ina volkano hai zaidi ya 100. Volkano nchini humo zina kiwango kikubwa cha maji katika magma, na hivyo, zinaweza zikasababisha milipuko mikubwa.
Mwanahabari wetu Janni Olsson anasikia kutoka kwa mtaalam wa volkano, Fujii Toshitsugu, kuhusu hali ya sasa ya volkano za Japani na tunachopaswa kufanya wakati wa mlipuko.
Mlipuko kwenye Mlima Fuji, nembo ya Japani, unasemekana kusababisha mkusanyiko wa majivu ya sentimita mbili hadi kumi jijini Tokyo. Hali hiyo inaweza kulemaza usafiri na miundombinu.
Maandalizi fulani yanahitajika kabla ya kutoka nje endapo mlipuko utazalisha majivu ya volkano.Vaa miwani na barakoa ya kuzuia vumbi ili kulinda macho yako na viungo vya mfumo wa upumuaji. Pia, vaa shati la mikono mirefu na suruali ili kuikinga ngozi yako dhidi ya majivu ya volkano.