Utayarishaji wa Mfuko wa Dharura
Ni muhimu kutayarisha mfuko wa kubeba wakati wa dharura ikiwa janga asili litatokea. Mtaalam anashauri kuhusu bidhaa na kiwango cha bidhaa za kuwekwa kwenye mfuko huo na pia mahali pa kuuhifadhi, ili tuweze kuuchukua haraka wakati tukihama.
Mifuko ya dharura ya wanachama watatu wa familia. Mfuko mmoja unapaswa kutayarishwa kwa kila mwanachama, endapo familia hiyo itatenganishwa wakati wa uhamaji. Hakikisha pia unaandaa helmeti ya kusaidia kukinga kichwa chako.
Vitu vya kuwekwa kwenye mfuko wa dharura vinaweza vikagawanywa katika makundi matatu. La kwanza linajumuisha vitu muhimu vya kuhakikisha uhai wako kama vile chakula na dawa. La pili ni bidhaa muhimu za matumizi kama vile tochi na shashi. Kundi la tatu linajumuisha vitu ambavyo ni vigumu kuvipata mara tu vipoteapo, kama vile nakala za vyeti vya ukaazi au orodha ya namba za simu za watu unaojuana nao.
Mizoguchi Nobuko, mshauri wa uzuiaji wa majanga na mpangaji mkuu wa kuhifadhi bidhaa za dharura, anatufunza hoja muhimu za kutayarisha mifuko ya dharura.