Virusi vya korona: maswali na majibu

Orodha ya maswali

172. Kwa nini chanjo ni muhimu?

Chanjo inalenga kuwapa watu kingamaradhi ama kuimarisha mifumo yao ya kinga. Inatarajiwa kuzuia watu kupata dalili kali ama kuugua sana. Mbali na hilo, pia inatarajiwa kudhibiti ueneaji wa ugonjwa huo katika jamii.
Wizara ya Afya ya Japani inasema matokeo ya majaribio ya kitabibu yaliyofanyika nje ya nchi, yameonyesha kuwa chanjo za virusi vipya vya korona, zinafaa katika kuzuia hali na dalili mbaya kama vile homa.
Ikiwa utoaji chanjo kwa watu wengi unaweza kusaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaougua sana, na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo, mzigo kwa mfumo wa huduma ya afya utapungua.
Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Februari 2. Inaweza kupatikana katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

171. Utoaji chanjo kwa raia wa kigeni wanaoishi nchini Japani.

Raia wa kigeni wanaoishi nchini Japani wanaweza kupata chanjo ya virusi vya korona katika manispaa walikojiandikisha kama wakazi.

Mpango wa utoaji chanjo nchini Japani umepangwa kuanza Februari 17. Chanjo hizo zitatolewa kwanza kwa wafanyakazi wa tiba, na kwa taratibu wanaopewa kuongezwa kwa kuwachanja wazee, wakifuatwa na watu walio na matatizo ya kiafya na wengineo.

Utoaji chanjo kwa wazee unatarajiwa kuanza wakati fulani mwezi Aprili.

Kuhusu mahali pa kupata chanjo, maeneo ya utoaji chanjo kimsingi, yatawekwa katika manispaa walikojisajili watu kama wakazi.

Serikali inapanga kutuma kuponi zinazohitajika kwa watu kupokea chanjo, wakiwa katika makazi yao. Chanjo hizo zinatolewa bila malipo.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Februari 15.

116. Hatua za kujilinda dhidi ya maambukizi ya mara nyingine.

Jitihada katika viwango vyote zinaendelea za kufanya chanjo zipatikane hivi karibuni. Lakini wataalamu wanaonya tusibweteke. Wanatutaka kuendelea na utekelezaji wa hatua za msingi, ikiwemo kunawa vizuri mikono, kuepuka kinachoitwa 3Cs--- “crowded places” yaani maeneo yenye watu wengi, “close-contact settings” yaani maeneo yenye nafasi ndogo na “confined and enclosed spaces” yaani maeneo yenye mzunguko mdogo wa hewa--- pamoja na kutokaribiana.

Ripota wa NHK wanaoangazia virusi vipya vya korona wanasema bado kuna mambo mengi tusiyoyajua kuhusu virusi hivyo. Wanasema kwamba tunapaswa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya tafiti mbalimbali. Lakini wanasisitiza kuwa ni muhimu kwetu kuendelea kuchukua hatua za msingi kwa kina.

115. Namna ya kukabiliana na kirusi hiki kigumu ambacho hakioneshi dalili ya kutoweka.

Matsuura Yoshiharu, Profesa katika Chuo Kikuu cha Osaka na Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Virusi nchini Japani, anasema tunapaswa kuwa na makisio kwamba maambukizi ya mara nyingine yanawezekana kama tu inavyotokea kwa virusi vya korona vya kawaida vinavyosababisha mafua, na kusababisha maambukizi ya kujirudia. Profesa Matsuura anasema kuwa kirusi kisichasababisha maambukizi ya kujirudia ni nadra sana. Pia anasema kwamba virusi haviwezi kuishi kama vitamuua mwenyeji wao. Historia ndefu kati ya binadamu na virusi inaonesha kuwa kadiri maambukizi yanavyojirudia, ndivyo dalili zinavyokuwa dhaifu. Profesa huyo amesema hatupaswi kuviogopa sana virusi.

114. Je, kuna chanjo zingine zozote fanisi? -2-

Tulimuuliza Profesa Sasaki Hitoshi wa Chuo Kikuu cha Nagasaki, anayefanyia kazi uendelezaji wa chanjo inayowezesha uzalishaji kingamwili kwenye utando laini uliopo mapafuni. Wakati virusi vinaponasa kwenye utando uliopo kwenye mapafu hayo, vinaweza kusababisha nimonia.
Chanjo hii inalenga kuzuia maambukizi ya virusi kwenye sehemu ya kuingia mwilini.

Imeundwa kwa chembe ndogo zisizo halisi zilizosanisiwa za RNA ya virusi vipya vya korona. Chanjo hii huvutwa ndani kupitia mdomoni, kwa hivyo inafika moja kwa moja kwenye utando laini wa mapafu. Watafiti wanaamini kwamba chanjo hii inaweza kuwa na ufanisi mkubwa kwa sababu inawezesha uzalishaji wa kingamwili katika sehemu ambayo virusi vinafanya kazi.

113. Je, kuna chanjo zingine zozote fanisi? -1-

Chanjo nyingi zimesanifiwa kutengeneza kingamwili kwenye mkondo wa damu. Lakini utafiti na uendelezaji pia unaendelea kuhusiana na chanjo zinazosaidia mwili kuzuia maambukizi.

Profesa Katayama Kazuhiko wa Chuo Kikuu cha Kitasato, anafanyia kazi aina mpya ya chanjo ya kupuliza puani. Kwa kuiweka chanjo hiyo puani, anaamini kuwa kingamwili zinaweza kubuniwa kwenye sehemu ya juu ya mfumo wa upumuaji na virusi vinaweza kuzuiwa kwenye sehemu ya kuingilia mwilini. Anasema amenuia kuendelea na utafiti katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo.

Profesa Katayama anasema iwapo kingamwili za immunoglobin-A zinaweza kutengenezwa kwenye tando laini za pua, maambukizi yanaweza kukomeshwa kabla ya virusi kuzaliana kwa idadi kubwa, hivyo virusi vinaweza kuzuiwa kufikia mapafu.

112. Uhusiano kati ya matukio ya kuambukizwa tena na ufanisi wa chanjo zinazotengenezwa hivi sasa.

Ni muhimu kutathmini maambukizi ya mara ya pili kwani yanaweza kushawishi utengenezaji wa chanjo. Chanjo zinalenga kutoa kingamaradhi kwa magonjwa ambukizi kwa kutoa hali dhaifu ya virusi na kuchochea mwili kutengeneza kingamwili. Hata hivyo, kuna maswali yanayohusu ufanisi wa chanjo ikiwa watu walioambukizwa waliozalisha kingamwili, wanaambukizwa tena.

Profesa Nakayama Tetsuo ni Mwanavirolojia katika Chuo Kikuu cha Kitasato. Anaonya watu kutokuwa wepesi wa kufikia hitimisho kwamba, chanjo hazifanyi kazi kwa sababu tu ya watu kuambukizwa tena. Nakayama anasema ingawa maambukizi ya mara ya pili yanawezekana hata baada ya chanjo kutengenezwa na kutolewa, kuna faida za kupewa chanjo.

Nakayama anasisitiza kuwa chanjo hazilengi tu kutoa uhakika wa kuzuia maambukizi, lakini zinadhaniwa kuwa na matokeo mengine, ikiwa ni pamoja na kuzuia wagonjwa kupata dalili kali.

111. Je, tunaweza kuzuia kuambukizwa tena?

Tulimuuliza Profesa Katayama Kazuhiko wa Chuo Kikuu cha Kitasato, aliyetuambia kwamba ni vigumu kuzuia watu kuambukizwa tena.

Virusi vya korona vinaingia mwilini mwetu kupitia utando laini uliopo juu ya njia ya mfumo wa upumuaji, inayohusisha pua na koo. Baadaye, kingamwili iitwayo “Immunoglobulin A, au IgA”, hutengenezwa kwenye utndo huo kupambana na virusi vinavyoingia.

Hata hivyo Katayama anasema kiwango hicho cha IgA huwa na tabia ya kupungua katika kipindi kifupi baada ya mtu kuambukizwa virusi na kuzalisha kingamwili. Hii ndiyo sababu ya yeye kusema tuna nafasi ndogo ya kuzuia virusi vya korona mpakani mara ya pili.

Katayama amepanga kuanzisha mradi wa utafiti kubaini kiwango cha IgA kinachozalishwa kwenye sehemu ya juu ya njia ya hewa kwa mtu aliyeambukizwa na hudumu kwa muda gani. Mradi huu unaweza kutoa mwanga juu ya swali letu, maambukizi ya mara zingine hutokea mara ngapi?

110. Iwapo dalili za maambukizi ya mara ya pili ni kali au la.

Wataalam wanasema kuwa, kwa virusi vya aina zingine nyingi mbali na virusi vya korona, dalili za maambukizi ya mara ya pili huwa si kali au wakati mwingine hakuna kabisa dalili yoyote

Mfano mzuri ni virusi viitwavyo “Respiratory Syncytial (sin-si-kchio)” au RSV vinavyosababisha dalili kama za mafua, lakini ambavyo pia vinapowapata watoto wadogo katika visa kadhaa vinaweza kuleta madhara zaidi na kusababisha nimonia na ugonjwa mkubwa.

Profesa Nakayama Tetsuo wa Chuo Kikuu cha Kitasato, alichunguza kingamwili za watoto 91 walioambukizwa virusi vya RSV. Kwa kawaida miili yetu hutengeneza kingamwili inaposhambuliwa na virusi ili kujaribu kuondoa virusi hivyo mwilini. Inaaminika kuwa, wakati kingamwili za kutosha zinapotengenezwa, mwili unaweza kujikinga na maambukizi.

Utafiti wa Profesa Nakayama ulibaini kuwa, wakati mtoto wa mwaka mmoja anapoambukizwa virusi hivyo, ni kiasi kidogo tu cha kingamwili kinachozalishwa. Ilibainika kuwa, kiwango cha kingamwili kiliongezeka baada ya maambukizi ya mara kadhaa.

Utafiti huo ulibaini kuwa, kadiri kiwango cha kingamwili kinavyoongezeka mwilini, dalili za ugonjwa huzidi kuwa hafifu. Katika visa vingi, watu walioambukizwa virusi hivyo walikuwa na mafua yaliyotiririka pekee.

Hatahivyo kwa upande wa homa ya dengi, maambukizi ya mara ya pili yanaweza kusababisha dalili kali zaidi. Homa ya dengi ni ugonjwa unaoenezwa na mbu ambao huweza kusababisha homa kali pamoja na maumivu makali ya kichwa.

Hivyo basi, vipi kwa upande virusi vya korona? Profesa Nakayama anasema kuwa, inawezekana baadhi ya watu hawaonyeshi dalili yoyote na wala hawafahamu iwapo wameambukizwa virusi vya korona kwa mara ya pili. Anatoa angalizo kuwa hali hiyo inapaswa kufuatiliwa kwa umakini kwa kuwa dalili za maambukizi ya mara ya pili bado sio bayana.

109. Kuhusu watu walioambukizwa virusi hivyo, wakapona, na kisha kuambukizwa tena.

Visa kama hivyo vya watu kuambukizwa tena vimekuwa vikiripotiwa maeneo mbalimbali duniani. Huenda watu wamekuwa wakijiuliza iwapo kweli hilo linatokea, au iwapo chanjo itafanya kazi. Leo tutaangazia visa vya aina hiyo vilivyoripotiwa.

Watafiti katika Chuo Kikuu cha Hong Kong ndio waliokuwa wa kwanza ulimwenguni kuripoti mwezi Agosti mwaka huu juu ya kisa cha mtu aliyeambukizwa tena virusi hivyo. Walisema kuwa, walithibitisha kwamba mwanamume mwenye umri wa miaka 33 mara ya kwanza aliambukizwa virusi vya korona mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu, akapona, lakini akaambukizwa virusi hivyo kwa mara ya pili zaidi ya miezi minne baadaye.

Watafiti hao walisema kuwa mpangilio wa jeni za virusi viligunduliwa katika awamu hizo mbili za maambukizi ulitofautiana kwa kiasi fulani, kwahiyo hicho kilikuwa ni kisa cha kwanza kabisa ulimwenguni cha maambukizi ya mara ya pili yaliyothibitishwa kisayansi.

Baada ya ripoti hiyo ya watafiti wa Chuo Kikuu cha Hong Kong, makundi mengine ya watafiti kutoka Marekani, India na kwingineko yalitangaza kuwepo kwa visa kama hivyo.

Jarida la kisayansi la “Nature” limechapisha makala kuhusiana na visa vya watu kuambukizwa tena, na suala hilo linazidi kuvutia angalizo.

Tulimuuliza Profesa Nakayama Tetsuo wa Chuo Kikuu cha Kitasato ambaye ni mtaalumu wa virusi, iwapo kweli watu wanaweza kuambukizwa tena virusi vya korona.

Profesa Nakayama alisema kuwa, maambukizi kwa mara ya pili hutokea kwa virusi vya aina zingine, kwahiyo watu wanaweza pia kuambukizwa virusi vipya vya korona kwa mara ya pili.

98. Je, unaweza kuambukizwa virusi hivyo ukiwa kwa daktari wa meno?

Chama cha Madaktari wa Meno cha Japani kinasema zahanati za meno zimeweka njia anuai za kuzuia maambukizi, hivyo watu wasio na homa, kikohozi ama dalili zingine wanaweza kutibiwa kama ilivyo ada.

Watu wenye dalili kimsingi huombwa kujizuia kutaka kuchunguzwa na madaktari.

Lakini chama hicho kinasema baadhi ya visa vinaweza kuwa vya dharura ama hata vinavyotishia maisha kama vitaachwa bila kushughulikiwa, hivyo watu wanapaswa kwanza kuwasiliana na madaktari wao wa meno.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

97. Iwapo ni salama kusafiri kwenye ndege ama treni iyendayo kasi ya Shinkansen?

Ni kweli kwamba hakuna mzunguko mzuri wa hewa ndani ya mabehewa ya treni ama ndani ya ndege kama ilivyo katika sehemu za nje. Lakini abiria wengi walioabiri ndege au treni hawapigi kelele au kugombana.

Tulimuuliza Sakamoto Fumie wa Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luke. Yeye ni mtaalama wa hatua za kukabiliana na maambukizi. Anasema mtu hahitaji kuwa na wasiwasi zaidi kuhusiana na kupata maambukizi akiwa kwenye ndege ama treni alimuradi asalie kimya na kutokaribiana na abiria wengine.

Hata hivyo, Sakamoto anaongeza kuwa ingawa kuna hatari ndogo ya kuambukizwa wakati unaposafiri, unaweza kukabiliana na hatari kubwa ya maambukizi ikiwa utaenda kufurahia tafrija na kuzembea au kufanya mambo ya kipumbavu katika sehemu maalum iliyotengwa katika nyumba ya kupanga au hoteli unayoishi. Anasema tabia kama hiyo inaweza kusababisha maambukizi ya watu wengi, kwa hivyo mtu anapaswa kuwa mwangalifu zaidi ili kuepukana nayo.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

96. Iwapo kuna uwezekano wa kuambukizwa virusi hivyo kwenye mabwawa ya kuogelea ama mabafu ya umma.

Tumemuuliza Sakamoto Fumie wa Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka ambaye ni mbobezi wa hatua za kukabiliana na maambukizi. Sakamoto anasema mtu yoyote hapaswi kuhofia juu ya kuambukizwa kupitia mabwawa ya kuogelea au mabafu.

Hata pale maji yanapokuwa na virusi, yanaweza kuwa na viwango vidogo vya virusi. Sakamoto anasema kutumia bwawa la kuogelea ama mabafu ya umma kuna hatari kidogo.

Anasema, hata hivyo kunaweza kusababisha hatari ya maambukizi iwapo utagusa vitu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo ambavyo vimeguswa na watu wengi wasiotambulika. Anawashauri watu kutoshika nyuso, midomo, pua na macho yao kwa mikono yao kabla ya kunawa vizuri.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

95. Kula mbogamboga zinazouzwa kwenye supamaketi bila kuzipika ni salama?

Anasema kwa sasa kuna nafasi ndogo ya wewe kuambukizwa virusi vya korona kupitia vitu unavyokula.

Watafiti wametoa makisio kwamba watu waliambukizwa virusi vya korona katika soko moja nchini China, kupitia wanyama walio hai wanaouzwa sokoni hapo. Hata hivyo, Sakamoto anasema hii haimaanishi watu waliambukizwa virusi hivyo kwa kula chakula walichonunua sokoni hapo.

Anasema hatuhitaji kuogopa sana alimuradi tule vyakula vinavyouzwa kwenye supamaketi, vilivyowekwa katika mazingira bora ya usafi. Anasema tunaweza kuviosha tu kama tunavyofanya kawaida na kuvila.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

94. Iwapo tunahitaji kuweka masharti ya utumiaji wa sehemu za wazi pia.

Tulimuuliza Sakamoto Fumie wa Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luke ambaye ni mtaalam wa hatua za kupambana na maambukizi swali hili. Sakamoto anasema hatari ya maambukizi kwa kiasi fulani ipo chini katika sehemu za wazi, kwa sababu tofauti na mazingira ya ndani, kuna mzunguko wa hewa kila wakati.

Hata hivyo, Sakamoto anaongeza kuwa hata unapokuwa katika sehemu za wazi, hatari ya maambukizi inaongezeka kwa kiasi fulani, ikiwa unazungumza na mtu kwa karibu. Anasema vinginevyo, hauna haja ya kuogopa sana.

Pia anatushauri kuendelea kutokaribiana pale tunapokuwa pamoja na kula nje, kwa mfano, katika hafla ya kufurahia kuchanua kwa maua ya mcheri. Anasema hilo litapunguza zaidi hatari ya maambukizi ikiwa watu wasiojihisi vizuri, wataepuka kuhudhuria hafla kama hiyo.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

93. Je, tunapaswa kufanya nini iwapo mmoja wa wanafamilia ataambukizwa?

Kundi la wataalam wa magonjwa ambukizi akiwemo Profesa Kaku Mitsuo wa Chuo Kikuu cha Tiba na Dawa cha Tohoku, ametoa kitabu kidogo cha maelekezo kilichoorodhesha hatua maalum za kusaidia kuzuia ueneaji wa maambukizi.

Kinasema ni mtu mmoja tu anayepaswa kumhudumia mgonjwa wa virusi vya korona kwenye familia husika. Wahudumiaji wanapaswa kuvaa glavu, barakoa na kunawa mikono mara kwa mara. Wanapaswa kupima jotomwili lao mara mbili kwa siku na kujifuatilia iwapo wanazo dalili za aina yoyote.

Kinasema ili kuzuia kuenea kwa virusi, vyakula havitakiwi kuandaliwa kwenye sinia na vyombo havipaswi kutumiwa na watu wengi. Sahani zinapaswa kulowekwa kwenye vitakasa kwa walau dakika tano na baadaye vioshwe. Nguo ama matandiko ambayo huenda yakawa na majimaji ya mwili, zinapaswa kulowekwa kwenye majimoto ya nyuzi 80 za selisiasi kwa walau dakika 10 kabla ya kufuliwa.

Kitabu hicho pia kinasema ni muhimu kuruhusu hewa kuingia na kutoka kwenye vyumba kwa kufungua madirisha kwa dakika tano hadi 10 kila baada ya saa moja au mbili.

Kaku anasema kwamba watu wengi huenda wakawa hawajui nini cha kufanya kama wao ama familia zao zitaonyesha dalili za kuambukizwa, hivyo anatumai kuwa kitabu hicho kitafaa katika kupunguza hatari za maambukizi na kusaidia watu kujihisi salama katika maisha yao ya kila siku.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

92. Njia ipi sahihi ya kunawa mikono yetu?

Virusi vya korona, sawia tu na influenza na mafua mengine yanayosababishwa na virusi, vinaenea kupitia vitone vinavyotokana na upumuaji kama vile kukohoa na kupiga chafya. Hatua za uzuiaji zinazopendekezwa na Shirika la Afya Duniani, WHO za kupambana na virusi vya korona, zinajumuisha kunawa mikono, kufunika mdomo na pua yako unapokohoa au kupiga chafya, ambazo pia ni tahadhari za jumla zinazochukuliwa dhidi ya magonjwa ambukizi.

Unaponawa mikono yako, unapaswa kufanya hivyo kwa kutumia sabuni na maji yanayotiririka, ukichukua sekunde zisizopungua 20 kusugua mikono yako vilivyo, ikiwemo katikati ya vidole vyako na ndani ya kucha zako. Wakati hakuna sabuni na maji yanayotiririka, ni bora pia kutumia vileo na vitakasa vingine vya mkono. Virusi vinavyochukuliwa na mikono yako vitaingia mwilini mwako kupitia macho, mdomo na pua. Kwa hivyo, tafadhali usiguse uso wako hadi unawe mikono yako barabara.

Kobayashi Intetsu ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Toho anayejikita katika udhibiti wa maambukizi. Tulimuuliza hoja muhimu za unawaji mikono. Hiki ndicho alichotuambia.

“Mosi, tumia sabuni nyingi, na kwa uangalifu mkubwa sugua kila kidole. Osha vifundo vya mikono yako. Ikiwa utatumia kiwango kinachostahili cha sabuni, unapaswa kusalia na povu baada ya kusugua sehemu zote za mikono yako.

Unaweza ukatumia ama maji baridi au moto yanayotiririka kusuuza mikono yako. Ni bora kuikausha ukitumia karatasi safi ya taulo na kufunga maji bila kugusa moja kwa moja sehemu ya kufungia mfereji.

Unapokuwa huwezi kunawa mikono yako kwa sabuni na maji, tumia vitakasa vyenye kileo. Kiwango cha kitakasa unachotumia ni muhimu. Hakikisha unaisukuma hadi chini pampu ya kutolea kitakasa.”

Anasema ni muhimu kusugua kitakasa kwenye sehemu zote za mikono yako wakati bado nyevu, na kwamba kuisukuma pampu kikamilifu huhakikisha unapata kitakasa cha kutosha kufanya hivyo.

Taarifa hii inapatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

91. Unapaswa kufanya nini wakati mkazi wa jengo la majumui anapobainika kuambukizwa virusi vya korona?

Hali kama hii ilitokea kwenye jengo moja la majumui lililopo mjini Asahikawa mkoani Hokkaido. Bodi ya chama cha wakazi wa jengo hilo ilimuuliza Mizushima Yoshihiro ambaye ni naibu mwenyekiti wa Zenkanren jinsi ya kulitakasa jengo hilo. Zenkanren ni shirika lisilokuwa la kujipatia faida na ni shirikisho la kitaifa la vyama vya usimamizi wa majengo ya majumui.

Mizushima alitembelea kituo cha afya ya umma cha eneo hilo na kuuliza ikiwa kinaweza kutuma mfanyakazi wake kulitakasa jengo hilo. Lakini kituo hicho kilikataa ombi hilo kikisema jengo hilo ni mali inayomilikiwa kibinafsi na hawawezi wakalitakasa.

Hali hii iliwaacha wakazi wa jengo hilo na kazi ya kulitakasa. Tulimuuliza mfanyakazi wa kituo cha afya ya umma mjini Asahikawa tunachopaswa kuzingatia tunapolitakasa jengo wenyewe.

Kwanza kabisa, tunahitaji kuvitakasa vitu vilivyo katika maeneo yanayotumiwa pamoja vinavyoguswa mara kwa mara na watu kwa mkono, moja kwa moja. Vinajumuisha vitufe vilivyo kwenye kibodi ya kengele ya mlango wa jengo, vitufe vya eleveta, sehemu za kushika mikono kwenye ngazi, vitu vilivyo ndani ya mabafu yanayotumiwa na watu wengi, na vitasa vya kwenye milango ya kuelekea katika ngazi za dharura.

Wanasema hakuna haja ya kupuliza kitakasa hewani kwa sababu huenda virusi visielee hewani kwa muda mrefu.

Wanawashauri wasafishaji kulowesha karatasi za jikoni ikiwa na asilimia 0.05 ya mchanganyiko wa sodium hypochlorite na kupangusa kila uso wa kitu kwa uangalifu mkubwa.

Ni bora watu kutopuliza mchangayiko huo kwenye karatasi ya jikoni kwa sababu wakifanya hivyo, wasafishaji wanaweza kuvuta mvuke huo wenye madhara. Aidha kupuliza kusikowiana kunaweza kukaacha nafasi ndogo isiyoloweshwa na kitakasa kwenye karatasi, hali inayosababisha utakasaji usiokuwa bora.

Tafadhali kumbuka kuwa tunachokisema hapa kinastahili katika mantiki ya Japani. Vituo vya afya ya umma katika nchi zingine huenda vikaitikia hali sawia kwa namna tofauti.

Taarifa hii inapatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

90. Je, watoto wanapaswa kuvaa barakoa?

Takayama Yoshihiro kutoka Idara ya Magonjwa Ambukizi ya Hospitali ya Okinawa Chubu amekuwa akiisaidia serikali ya Japani kuandaa mikakati ya kukabiliana na virusi vya korona. Anatahadharisha dhidi ya kuvalisha watoto barakoa akisema huenda wakagusa nyuso zao mara kwa mara wanapovaa barakoa na hiyo itaongeza hatari ya maambukizi. Takayama anasema inapokuja kwa watoto, hatua za msingi kama vile kunawa mikono mara kwa mara na kuangalia halijoto yao wanapoondoka na kurejea nyumbani zinapaswa kupewa kipaumbele.

Chama cha Madaktari wa Watoto nchini Japani kinapendekeza watoto chini ya umri wa miaka miwili kutovaa barakoa kikisema inaweza ikawafanya kupata ugumu wa kupumua. Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi pia inasema haitoi ombi kwa raia wote kuvaa barakoa kwani baadhi ya watoto wanapata shida kuvalia barakoa itakikanavyo.

Takayama anawatahadharisha wazazi kuhusiana na kuwalazimisha watoto wao kuvaa barakoa kwa sababu tu watoto wengine wanaivaa. Anawarai wazazi kuchukua hatua za msingi na kuzingatia hatua za ukuaji wa watoto wao wanapoamua ikiwa wanapaswa kuvaa barakoa au la.

Taarifa hii inapatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

88. Maendeleo ya utengenezaji wa dawa ya kutibu virusi vya korona.

Zaidi ya miezi sita imepita tangu Machi 11 pale Shirika la Afya Duniani WHO lilipotambua kuwa maambukizi yalikuwa janga la dunia. Leo mada yetu inazungumzia maendeleo ya utengenezaji wa dawa ya kutibu virusi vya korona.

Kwa sasa hakuna dawa ambayo inaweza kuelezewa kama “dawa ya maajabu” kwa virusi vya korona. Hata hivyo, maendeleo yamepigwa katika kutafuta dawa, iliyotengenezwa kutibu magonjwa mengine, ambayo pia inaonyesha ufanisi katika kutibu virusi vya korona. Katika miezi sita, mengi yamebadilika katika juhudi za kutengeneza tiba ya virusi vya korona tangu mlipuko huo ulipoelezewa kama “janga.”

Katika siku za mwanzo kilikuwa na dawa ambazo mwanzoni zilionekana kuwa na matumaini, lakini ufanisi ambao haukuthibitishwa. Moja ya hizo dawa ilikuwa dawa ambayo inafifisha dalili za UKIMWI. Kilikuwa na matumaini kuwa utaratibu ambao unazuia virusi vya UKIMWI kuzaliana pia ungesaidia kutibu virusi vya korona. Hata hivyo, matokeo ya majaribio ya kitabibu yaliofanywa nchini China na Uingereza yalionyesha dawa hiyo haikupunguza kiwango cha vifo kwa wagonjwa waliougua zaidi na virusi vya korona.

Dawa nyingine ambayo ilionekana kuonyesha matumaini ilikuwa hydroxycholoquine ambayo inatumika kutibu malaria. Hata hivyo Idara ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) mnamo mwezi Juni ilitengua kibali cha matumizi ya dharura ya dawa hiyo kwa ajili ya kutibu virusi vya korona, ikisema vipimo havikuonyesha kwamba dawa hiyo ilikuwa na ufanisi wa kutibu ugonjwa wa COVID-19.

Kwa upande mwingine kuna dawa zingine ambazo zimethibitishwa kufanywa kazi kwenye virusi vya korona. Hizi ni pamoja na remdesivir, ambayo ilitengenezwa kutibu Ebola. Majaribio yaliyofanyika nchini Marekani yalithibitisha dawa hiyo ilikuwa na ufanisi katika virusi vya korona. Mwezi Mei, ilikuwa dawa ya kwanza kuidhinishwa kutibu virusi vya korona nchini Japani.

Ufanisi wa steroid dexamethasone katika kupunguza kiwango cha vifo pia kimethibitishwa katika utafiti nchini Uingereza. Dawa hiyo pia ilianza kutumika katika tiba nchini Japani.

Miezi sita iliyopita, ufanisi wa kutibu virusi vya korona ulikuwa haujulikani. Wizara ya afya na ustawi wa jamii hivi sasa inashauri dawa hizo mbili katika miongozo yake ya kutibu virusi vya korona.

Kuna dawa zingine ambazo zinatengenezwa na zinafanyiwa majaribio ili kuthibitisha ufanisi wake.

Kampuni ya kutengeneza dawa ya Japani ambayo ilitengeneza dawa ya kutibu mafua ya Avigan, kwa mfano, inafanya majaribio yenye lengo la kupata idhini ya serikali kwa ajili ya matumizi ya dawa hiyo kama tiba ya virusi vya korona. Majaribio ya kitabibu pia yanafanywa kwenye dawa ya Actemra, ambayo inatibu ugonjwa sugu unaoathiri viungo. Dawa zingine zinazoonyesha matumaini ni pamoja na Alvesco, dawa ya kutibu pumu, na Futhan ambayo kawaida inatumika kutibu ugonjwa wa kongosho. Ikiwa ufanisi na usalama utathibitishwa, kuna matumaini kwamba dawa hizo pia zitatumika kutibu virusi vya korona.

Morishima Tsuneo wa Chuo Kikuu cha Kitabibu cha Aichi ambaye ni mtaalam wa magonjwa ambukizi, anasema watafiti wamefahamu kuhusiana na asili ya magonjwa katika kipindi cha nusu mwaka iliyopita na tiba kadhaa zenye ufanisi zimegundulika. Sababu hizo zimechangia kupunguza kiwango cha vifo vinavyotokana na virusi katika wimbi la pili la mlipuko huo nchini Japani.

Taarifa hii inaweza kupatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

82. Unawezaje kupata maambukizi?

Mbali na kupitia vijitone vya mfumo wa upumuaji, virusi hivyo vinaweza kuambukizwa kwa njia ya kutogusa moja kwa moja.

Maambukizi kwa njia ya kutogusa moja kwa moja inaweza kutokea ikiwa mtu atagusa kitu baada ya mtu aliyeathirika. Mara nyingi watu hugusa nyuso zao pamoja na pua na midomo yao kila siku za maisha yao, na ikiwa watafanya hivyo kwa mikono iliyogusa virusi, wanaweza kupata maambukizi. Macho pia yanaweza kuwa njia ya kupata maambukizi, hivyo watu wanaweza kuathirika kwa kusugua macho yao.

Vijitone vidogo mno vinaaminika kusambaza virusi hivyo. Ni vidogo kuliko vitone na huelea hewani katika sehemu zenye mzunguko mdogo wa hewa. Ili kuzuia maambukzi kutokana na vijitone hivyo, watu wanashauriwa kuepuka C tatu. Closed poorly ventilated spaces yaani maeneo madogo yenye mzunguko finyu wa hewa, Crowded areas yaani maeneo yenye watu wengi na Conversation in close proximity yaani kufanya mazungumzo kwa umbali mdogo. Kwa kawaida vijitone vinasemekana kuanguka kabla ya kufika umbali wa kama meta 2, hivyo kudumisha angalau umbali huo baina ya watu inadhaniwa kuwa salama.

Si kila kitu kinajulikana kuhusu kusambaa kwa virusi hivi vipya. Ila kwa sasa hatua zipo kwa matumaini kuwa tunaweza kuzuia maambukizi kwa kuepuka kabisa vijitone na kutogusa virusi hivyo.

Ili kupunguza hatari ya maambukizi kote Japani mamlaka zinatoa wito kwa kila mmoja kuvaa barakoa, ili kuepuka kusambaa kwa vijitone, na kukaa umbali wa angalau meta 2 kila mmoja ikiwa kuna vijitone. Watu pia wanashauriwa kunawa mikono, ili wasijiambukize ikiwa wamegusa sehemu zenye virusi hivyo kwa mikono yao na kushika mdomo, pua au macho yao bila kujua.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japani.

80. Kumekuwa na aina ngapi za virusi vya korona tangu awali ambavyo binadamu anaweza kuambukizwa?

Zimepatikana zaidi ya aina 50 za virusi vya korona. Aina sita kati ya hizo zinaambukizwa kwa binadamu. Nne kati ya sita hizo kwa kawaida zinagunduliwa kama mafua.

Watu wengi wanaaminika kupata moja au zaidi ya aina hizo nne za virusi vya korona wakati wa utoto wao.

Aina mbili zinazobaki ni SARS na MERS. Aina hizi mbili zinaonesha dalili kali kulinganisha na zile nne. Wataalamu wanasema wakati wa mlipuko wa aina hizo virusi sumbufu viliibuka.

Mwishoni mwa mwezi wa 12 mwaka jana, mamlaka za China zilichunguza visa vya homa ya mapafu huko Wuhan. Huo ndio wakati walipogundua aina ya saba ya virusi vya korona ambayo ilikutwa kwa binadamu, na kufahamika kama virusi vipya vya korona.

Wataalamu wengi walitarajia kwamba virusi hivi vipya kuibuka, lakini isingekuwa kitu cha kusumbua kama hivi.

Kama ilivyotajwa awali, aina nne ni mafua ya kawaida. SARS ilidhibitiwa kwa ufaulu kwa kuwa dalili zake ziligunduliwa kirahisi, na MERS haikuwa janga.

Hivyo watu hawakuwa katika tahadhari. Iliaminika kuwa hata kama virusi vipya vya korona vingeibuka, vingedhibitiwa au visingesambaa sana.

Kulikuwa na vitabu vilivyoonya hatari ya virusi vipya vya korona vitakavyosababisha janga. Lakini si wataalamu wengi duniani waliodhani ni kweli.

Taarifa hii inaweza kuthibitishwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japani.

79. Kwa nini virusi vipya vya korona vinasambaa maeneo mengi na kwa haraka?

Kwa sasa hakuna chanjo dhidi ya virusi hivi vipya vya korona. Ni kwa kiasi gani virusi vinaambukiza inaweza kutathminiwa kwa wastani wa idadi ya watu waliopata maambukizi kwa mara ya kwanza kutoka kwa mtu aliyeathirika. Mathalani, ikiwa mtu mmoja aliyeathirika ataambukiza virusi kwa wastani wa watu 0.5, ina maana virusi sio vya kuambukiza san ana huenda visisambae katika maeneo mengi. Lakini virusi hivi vipya vya korona, vinaaminika kwamba mtu mmoja aliyeathirika anaweza kuambukiza karibu watu 2.5.

Hata hivyo jopo la wataalamu linaloishauri serikali ya Japani juu ya virusi vya korona, linaamini kuwa haimaanishi kila mtu mmoja aliyeathirika anaambukiza watu 2.5. wataalamu wanasema kama kuna waathirika 10 wa virusi hivyo, wanane kati yao huenda wasimwambukize yeyote, wakati wawili wanaosalia wanaambukiza virusi kwa karibu watu 10 kila mmoja.

Tatizo lingine ni kuwa si rahisi kuwatambua waathirika wa virus vya korona. Watu walipoambukizwa virusi vya SARS, ambayo ni aina nyingine ya virusi vya korona, walipata dalili haraka hivyo watu wengine waliwajua wameathirika. Watu walioathirika wanaweza kutengwa ili kuzuia ueneaji wa virusi hivyo kwa wengine.

Lakini waathirika wa virusi vya korona wanaweza kueneza virusi hata kama hawaoneshi dalili, na hilo linafanya kuwa vigumu kuzuia ueneaji wa virusi hivyo.

Taarifa hii inaweza kupatikana pia katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japani.

78. Yapi ni maadili mazuri ya kukohoa? Na ninapaswa kuzingatia nini ninaponawa mikono?

Virusi vya korona, sawa tu na virusi vya influenza na mafua huenea kupitia vitone vinavyotolewa wakati mtu aliyeambukizwa anapokohoa au kupiga chafya.

Shirika la Afya Duniani, WHO linawataka watu kunawa mikono mara kwa mara na kuzingatia “maadili ya kukohoa” ili kuzuia ueneaji wa virusi hivyo. Hatua hizo ni sawa na zile zilizochukuliwa kukabiliana na magonjwa mengine ambukizi.

Wakati unaponawa mikono, tumia sabuni na maji ya kutiririka. Tumia sekunde zisizopungua 20 kusafisha juu ya mikono yako yote, ikiwa pamoja na katikati ya vidole na chini ya kucha. Ikiwa hakuna sabuni na maji, safisha mikono yako kwa kutumia vitakasa vya kileo.

Unaweza ukaambukizwa virusi hivyo ikiwa utagusa macho yako, mdomo na pua kwa mikono michafu. Hakikisha haugusi uso wako kabla ya kunawa mikono.

Ikiwa una dalili kama vile kukohoa au kupiga chafya, usikose kuzingatia “maadili ya kukohoa” yafuatayo, ili usiwaambukize watu walio karibu nawe hata ikiwa umeambukizwa.

Funika mdomo wako kwa tishu au uuweke chini ya kiwiko cha mkono wako wakati unapokohoa au kupiga chafya. Ukitumia tishu, itupe punde baada ya kuitumia na unawe mikono. Usifunike mdomo kwa viganja vya mikono yako kwa sababu vitaambukizwa virusi hivyo.

Taarifa hii inapatikana kwenye tovuti ya NHK World Japan na mitandao ya kijamii ya NHK.

77. Je, nilisikia kwamba si rahisi kufanyiwa vipimo vya PCR nchini Japani. Ni kwa nini?

Vipimo vya PCR hutambua nyenzo za jeni ya pathojeni na kubaini ikiwa mtu huyo ameambukizwa wakati huo. Ni vipimo ambavyo matokeo yake huwa sahihi sana lakini yanachukua muda. Inasemekana kwamba Japani haifanyi vipimo vingi vya PCR kama nchi zingine. Hii ni kwa sababu imekuwa na fursa chache za kufanya vipimo hivyo kabla ya mlipuko wa virusi vipya ya korona.

Mojawapo wa sababu ni kwamba Ugonjwa Hatari Unaoathiri Mfumo wa Upumuaji, yaani SARS au Ugonjwa Hatari Unaothiri Mfumo wa Upumuaji wa Mashariki ya Kati, yaani MERS. Haya yote yakiwa ni magonjwa yanayohitaji vipimo vya PCR, hayakuathiri Japani. Na inapokuja kwa suala la influenza, vifaa rahisi vya kufanyia vipimo vinatumika pakubwa, kwa hivyo vipimo vya PCR vimetumika kwa nadra mno nchini Japani.

Kwa sasa matumizi ya vipimo hivyo yanaongezwa kwa taratibu, lakini bado havijafikia kiwango ambapo vinaweza vikaenea haraka, na hiyo inasemekana kuwa changamoto.

76. Jinsi ya kuhakikisha vyumba vyako vina hewa safi itakikanavyo.

Kampuni ya kutengeneza milango na madirisha ya YKK AP pia imezungumzia na kujibu swali la jinsi ya kuhakikisha vyumba vyako vina hewa safi itakikanavyo.

Kwenye tovuti yake, kampuni hiyo inaorodhesha mapendekezo ya namna unavyopaswa kuhakikisha vyumba vyako vina hewa safi kwa kufungua madirisha itakikanavyo, katika muktadha wa virusi vipya vya korona.

Kampuni ya YKK AP inapendekeza “ufunguaji wa madirisha mawili badala ya moja”, na kwamba madirisha hayo yanapaswa kufunguliwa “yakikinzana kwa mshazari.”

Katika vyumba viliyo na dirisha moja tu, kampuni hiyo inapendekeza ufunguaji wa milango ya ndani ili kutengeneza njia ya kupitisha hewa, na kutumia feni kuzungusha hewa.

Kadhalika kampuni hiyo inapendekeza kuyafungua madirisha kwa kuyasogeza hadi katikati ili yafunguke pande zote.

Unaweza ukaipata taarifa hii kwenye tovuti ya NHK World Japan na mitandao ya kijamii ya NHK.

75. Unaweza ukahakikisha vipi kuna hewa safi katika vyumba wakati unapotumia viyoyozi?

Kampuni kubwa ya utengenezaji wa viyoyozi ya Daikin Industries inasema viyoyozi vingi huzungusha tu hewa katika chumba wala havihakikishi uwepo wa hewa safi. Kampuni hiyo sasa inawataka watu nyakati zingine kufungua madirisha yao na kuhakikisha hewa safi inaingia katika vyumba hivyo, wanapokuwa wamewasha viyoyozi vyao.

Baadhi ya watu huenda wakahisi kuwa wanatumia vibaya umeme ikiwa watafanya hivyo. Afisa mmoja alielezea njia ya kudhibiti matumizi ya umeme wakati ukipitisha hewa safi chumbani. Kwa sababu viyoyozi hutumia umeme mwingi unapoviwasha, unapaswa kwa kweli kuhakikisha vimewashwa wakati ukifungua dirisha lako.

Katika hali za joto kali, matumizi ya umeme pia yataongezeka ikiwa hewa nyingi kutoka nje itasababisha halijoto ya chumbani kupanda, kwa hivyo ni muhimu kupandisha kidogo halijoto ya kiyoyozi chako kabla ya kufungua dirisha ili kuruhusu hewa safi kuingia chumbani.

Unaweza ukaipata taarifa hii kwenye tovuti ya NHK World Japan na mitandao ya kijamii ya NHK.

73. Miongozo ya ndani ya makampuni kwenye maeneo ya uzalishaji ambapo ni vigumu kuhamia kwenye ufanyaji kazi nyumbani.

Kampuni ya kutengeneza malori na basi ya Mitsubishi Fuso zimeweka miongozo ya kuzuia maambukizi kwa wafanyakazi waliopo sehemu za utengenezaji.

Katika kiwanda cha kampuni hiyo kilichopo mji wa Kawasaki karibu na Tokyo, wafanyakazi wanaombwa kukaa ama kusimama angalau umbali wa mita 1.5. Pale wanapohitaji kusimama karibu karibu, kwa mfano wanapobeba pamoja vitu vizito, wavae ngao za usoni juu ya barakoa kwa ajili ya majaribio.

Wafanyakazi wote wabadili glavu zao za kazi mara moja kila baada ya nusu siku, na kuweka vitakasa kwenye chumba cha makabati mara nyingi ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi.
NHK ilimuuliza afisa wa Mitsubishi Fuso Baba Takashi. Alisema kuchukua hatua za kuzuia maambukizi ni muhimu zaidi kwenye sehemu za utengenezaji wa malori ambapo ni vigumu kuwa na mifumo ya kujiendesha yenyewe na kazi nyingi zinafanywa kwa mikono.

Alisema mapambano dhidi ya virusi huenda yakaendelea kwa kipindi fulani na kwamba anataka kusikia mapendekezo kutoka kwa wafanyakazi na kuboresha mazingira ya kazi ili wafanyakazi wote waweze kufanywa kazi kwa usalama zaidi na furaha.

Kampuni ya Toyota Motor inayoongoza kutengeneza magari Japani, mwishoni mwa mwezi Machi ilichelewa kuanza zamu za jioni kwa nusu saa katika viwanda vyake vya utengenezaji vilivyopo mkoani Aichi. Hilo liliwapa wafanyakazi wa zamu ya mchana na ya usiku takribani dakika tisini ili kubadili na kupunguza nafasi ya wafanyakazi kukutana katika zamu mbalimbali.

Kampuni ya kutengeneza mashine nkubwa ya IHI Corporation iliwagawa wafanyakazi kwenye makundi mawili katika kiwanda chake cha kutengeneza injini za ndege kilichopo katika mji wa Mizuho mkoani Tokyo. Kila kundi linapaswa kufika kazini kila wiki ingine.

Kampuni nyingine ya kutengeneza malori ya Isuzu Motors iliongeza mara tatu idadi ya huduma za mabasi kwenye kiwanda chake cha Fujisawa mkoani Kanagawa wakati wa asubuhi wa kwenda kazini ili kuzuia msongamano kwenye mabasi.

Taarifa hizi inaweza kupatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

71. Miongozo ya kuzuia maambukizi iliyozinduliwa na sekta ya reli na usafiri wa anga.

Kwa mujibu wa miongozo ya kawaida iliyotolewa na mitungo ya kampuni za reli ikiwa ni pamoja na kampuni ya JR na makampuni mengine makubwa ya reli, waendeshaji wanashauriwa kuwaomba abiria kuvaa barakoa, kufanya kazi nyumbani ili kuzuia msongamano, na kuepuka usafiri wa umma nyakati za abiria wengi.

Waendeshaji wa reli pia wanashauriwa kuweka vitakasa kwa uangalifu na kufungua madirisha ili kuboresha uingiaji wa hewa.

Mbali na hilo, viti vilivyohifadhiwa kwenye treni isiyosimama vituo vyote vitapangwa kwa ajili ya abiria kukaa mbalimbali.

Wakati huo huo, miongozo iliyotolewa na Chama cha Kampuni za Usafiri wa Anga cha Japani inapendekeza kampuni za usafiri wa anga kuwaomba abiria kuvaa barakoa, na wafanyakazi kuweka vitakasa mara kwa mara ndani ya ndege. Kampuni pia zinashauriwa kutoa vinywaji vilivyofungashwa ndani ya ndege.

Miongozo kwa waendeshaji wa majengo ya uwanja wa ndege inayaomba makampuni kuanzisha njia za kuwaomba abiria kudumisha umbali baina ya mtu na mtu katika sehemu ya ukaguzi wa taarifa za usafiri na wakati wa taratibu za ukaguzi wa usalama. Waendeshaji pia wanaombwa kusafisha kwa uangalifu maeneo yanayoguswa mara kwa mar ana abiria kwa kutumia vitakasa.

Katika kaunta za ukaguzi wa taarifa za usafiri, vifaa vinavyowagawa mtoaji huduma na abiria vinaweza kuwekwa pale inapohitajika ili kuzuia kusambaa kwa matone ya mate. Halijoto ya mwili itaangaliwa kwa abiria yeyote anayejihisi vibaya.

Katika viwanja vikubwa sita vya ndege vya Japani ikiwa ni pamoja na Haneda, Narita na Kansai, halijoto ya mwili ya abiria itaendelea kufuatiliwa kwa kutumia themografia.

Taarifa hizi inaweza kupatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World Japan.

65. Virusi vya korona vinaweza kuambukizwa kabla mtu hajaonyesha dalili, kama vile homa na kikohozi?

Kundi moja la watafiti nchini Singapore linasema linaamini hali hiyo imetokea katika visa kadhaa. Watafiti hao walitafuta namna maambukizi yalivyotokea nchini Singapore na kutoa matokea yao katika ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Magonjwa Ambukizi nchini Marekani. Baada ya tathmini ya kina walibaini visa katika makundi saba ya maambukizi ambayo wanaamini usambaaji wake wa binadamu kwa binadamu umetokea kutoka kwa watu ambao hawakuonyesha dalili.

Watu wasio na dalili walianza kupata homa, kukohoa au kuwa na mafua kwa siku kadhaa baada ya kukutana na wengine ambao baadaye walipata virusi hivyo. Watafiti hao wanaamini watu wasio na dalili wameeneza maambukizi wakati ambapo hawakuwa na dalili kupitia vitone na njia zingine.

Baadhi ya maambukizi mengine ya kundi yametokea wakati wa masomo ya uimbaji. Watafiti hao wanasema hata ikiwa mtu alikuwa hakohoi, virusi hivyo vinaweza kuambukizwa kupitia vitone wakati wa kuimba kwa sauti kubwa au namna zingine.

Watafiti hao wanaamini hilo linathibitisha kwamba virusi hivyo vipya vya korona vinaweza kuambukizwa wakati ambao mtu hajaanza kuwa na dalili. Wanasema kuwatenga watu walioanza kuonyesha dalili pekee haitoshi, na ni muhimu kuepuka mikusanyiko na umati wa watu.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 20. Pia zinapatikana katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World JAPAN.

57. Baadhi ya watu huvaa barakoa bila kufunika pua. Wataalamu wanafikiria nini juu ya hili?

Lengo kuu la kuvaa barakoa ni kuzuia vitone vinavyotoka wakati wa kupumua ama kutoka kwa mfumo wa kupumua visisambae, na kuzuia kiasi kikubwa cha vitone vinavyotolewa na mwathirika. Ikiwa pua yako haijafunikwa, vitone vinavyotoka kwa njia ya chafya vitasambaa. Pia, binadamu avutapo pumzi, asilimia 90 ya hewa inayovutwa inavutwa kupitia pua, hivyo kutofunika pua kunaongeza hatari ya maambukizi.

Unapovua barakoa, unatakiwa kuhakikisha kuna umbali wa kutosha wa kimwili. Inasemekana kwamba vitone hivyo vinaweza kusambaa hadi karibu mita mbili. Kama hatua ya kuzuia kuzimia kutokana na joto kali, wizara ya afya ya Japani inapendekeza kuvua barakoa yako unapokuwa angalau umbali wa mita 2 kutoka mtu mwingine.

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya St. Luke nchini Japani anasema watu hawahitaji kuvaa barakoa wakati wote, isipokuwa inapokuwa na ulazima. Sakamoto anasema kuendelea kuvaa mara kwa mara barakoa kunasababisha hatari ya kupata ugonjwa wa kuzimia kutokana na joto kali.

Kuchagua aina ya kitambaa cha Barakoa pia ni muhimu, hususan katika miezi ya joto. Watu wengi wanatengeneza barakoa zao kwa vitambaa vya aina mbalimbali. Shirika la Afya Duniani linatoa taarifa juu ya ufanisi wa aina mbalimbali za vitambaa vya barakoa, kwa misingi ya uwezo wa kupumua vizuri na ubora wa kuchuja, ambapo ni uwezo wa kitambaa kuchuja vitone. Shirika hilo linasema nailoni ina ubora wa hali ya juu wa kuchuja lakini hutoa uwezo wa kupumua vizuri ni mdogo. Pamba inayotumika kwenye bendeji ni rahisi kupumua lakini ina ubora mdogo wa kuchuja. WHO inasema pamba inapaswa kuambatanishwa na aina nyingine ya kitambaa ili kuongeza ufanisi wake wa kuchuja.

Kundi moja la madaktari bingwa wa watoto linasema barakoa hazipaswi kuvaliwa na watoto walio chini ya miaka miwili kwa sababu ya hatari ya kushindwa kupumua.

Sakamoto wa Hospitali ya Kimataifa ya St. Luke anasema si tu kuvaa barakoa, bali pia ni muhimu kuchukua hatua za msingi za kujilinda kama vile kusafisha mikono na kuepuka kile kinachoitwa “C tatu” ambazo ni “Closed spaces” yaani maeneo yasiyo na nafasi kubwa, “Clowded places” yaani maeneo yenye watu wengi na “Close contact” yaani kukaa karibu.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 8. Pia inapatikana katika tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK World JAPAN.

56. Unaoshaje barakoa za vitambaa?

Jibu. Kitu cha msingi ni kutozisugua.
Wizara ya afya ya Japani inasema kwanza unapaswa kuziloeka barakoa za vitambaa kwenye beseni lenye maji na sabuni kwa takribani dakika 10. Kiwango cha sabuni kinategemea na aina ya sabuni hiyo lakini kawaida, unaweza kuhitaji gramu 0.7, ama takribani nusu ya kijiko kwa kila lita mbili za maji. Kisha osha barakoa kwa kugandamiza kidogo na mikono yako. Suuza vizuri barakoa kwa maji kwenye beseni.

Kama unataka kutumia mashine ya kufulia, weka barakoa kwenye wavu ambao una ukubwa sawa na barakoa. Kausha maji yoyote yaliyozidi kwenye barakoa kwa kutumia taulo safi na anika kwenye kivuli.

Wizara hiyo imesema ni bora kuosha barakoa mara moja kwa siku na kushauri kutozitumia tena ikiwa hazitarudi katika umbo lake.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 6 na inaweza kuthibitishwa kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK WORLD Japan.

55. Wataalam wa afya wanavalia barakoa. Lakini nasikia habari za wauguzi na madaktari kuambukizwa virusi vya korona. Je, barakoa hakika zinafaa katika kuzuia maambukizi?

Haijabainika ikiwa barakoa zinaweza kuzuia maambukizi. Hata hivyo, barakoa zinazovaliwa sana na watu wengi mara moja na kisha kutupwa hazizuii virusi kikamilifu, kwa hivyo kufaa kwake katika kuzuia maambukizi kunaaminika kuwa na ukomo hata ikiwa zinafaa.

Katika mazingira ya afya, wafanyakazi huvaa barakoa sambamba na hatua zingine za kujikinga zinazotokana na ufahamu wa kitaalam. Hata hivyo, inasemekana kwamba barakoa pekee hazitoi kinga kubwa dhidi ya maambukizi.

Barakoa aina ya N95 ni barakoa za kitabibu zenye utendaji kazi wa kiwango cha juu ambazo wafanyakazi wengi wa afya huzivaa kwenye chumba cha kulaza wagonjwa mahututi. Zinaweza kuchuja virusi lakini zinaweza zikafanya iwe vigumu kwa aliyezivaa kupumua.

Kwa matumizi sahihi ya barakoa za N95, ni muhimu kujifunza awali namna sahihi ya kuzivaa na kuzitumia. Haijalishi ni aina gani ya barakoa unayovaa, kushika uso wako kabla ya kuitakasa mikono yako kunaongeza athari ya kuambukizwa.

Kwa upande mwingine, zikivaliwa na mtu aliyeambukizwa virusi vya korona, barakoa zinasemekana kupunguza kwa kiasi kikubwa athari ya mtu kueneza virusi hivyo kwa wengine.

Hadi sasa, inafahamika kuwa virusi vya korona kimsingi vinaambukizwa kupitia vitone vinavyotokana na upumuaji. Pia inafahamika kwamba mtu aliyeambukizwa virusi vya korona hutoa kiasi kikubwa cha virusi hivyo kuanzia takribani siku mbili kabla ya kuanza kuonyesha dalili, hadi mara tu baada ya kuonyesha dalili za virusi hivyo.

Inasemekana kuwa uvaaji wa barakoa huzuia kwa kiasi kikubwa kutawanyika kwa vitone vinavyotokana na kukohoa na kupiga chafya, pamoja na vitone vidogo zaidi ambavyo ni chembe ndogo sana zinazotolewa wakati watu wanapozungumza.

Omi Shigeru ni naibu mkuu wa jopo la wataalam la serikali ya Japani. Akiongea na waandishi wa habari mwezi Mei mwaka huu, Omi alisema anataka kila mmoja bila kujali ikiwa wana dalili za maambukizi au la, kuvaa barakoa ili kupunguza athari ya kuenea kwa virusi hivyo.

Alisema ingawa pamekuwepo na maoni mbalimbali kuhusiana na matumizi ya barakoa, makubaliano ya jumla yanaafikiwa katika mataifa mengine na pia kwenye Shirika la Afya Duniani.

Usahihi wa taarifa hii ni wa kufikia hadi Julai 3.

54. Kuna uhusiano wowote kati ya iwapo mtu ana kingamwili ama la na iwapo mtu huyo kwa sasa ana virusi vya korona au la kwenye kipimo cha PCR?

Kwanza tutupie macho juu ya kipimo cha kingamwili. Upimaji kingamwili hufanyika kubaini iwapo mtu anayo aina ya protini iitwayo “kingamwili,” zinazotengenezwa kwa seli za kujikinga kwenye damu pale zinapopambana na virusi vinavyoathiri damu. Katika upimaji, matone machache ya damu huchukuliwa, na sampuli hiyo huwekwa kwenye kifaa cha kupimia. Hata hivyo, unapaswa kufahamu kwamba kutengenezwa kwa kingamwili huchukua muda na haziwezi kugunduliwa mapema baada ya kuambukizwa.

Taasisi ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Japani ilichunguza sampuli za damu za wale walioambukizwa virusi vya korona kwa kutumia vifaa vya kupimia kingamwili vinavyouzwa madukani. Walibaini kuwa katika sampuli nyingi ilikuwa si chini ya wiki mbili baada ya mhusika kuanza kuonyesha dalili za kuambukizwa ndipo kingamwili zilibainika.

Sasa hebu tuangazie kipimo cha PCR. Kipimo hiki kinabaini iwapo umeambukiwa ama la. Iwapo kipimo kitasema umeambukizwa, hiyo itamaanisha una virusi hivyo mwilini mwako. Hata hivyo, mara nyingi hutokea kwamba kingamwili huwa hazibainiki kwa kuwa huwa hazijatengenezwa bado. Kwa upande mwingine, kipimo cha PCR kikisema hakuna virusi, hiyo kwa kiasi kikubwa humaanisha hujaambukizwa bado. Ama inaweza kumaanisha kwamba virusi vimeondoshwa kutoka mwilini mwako baada ya kuwa uliambukizwa. Kwa kisa cha virusi kuondolewa mwilini kuna uwezekano wa kubainika kuwepo kwa kingamwili mwilini mwako katika kipimo cha kingamwili.

Wakati huo huo, aina mpya ya kipimo imekuwa ikitengenezwa. Aina hii mpya ya kipimo inatarajiwa kubaini aina nyingine ya kingamwili inayoafahamika kuonekana kwenye damu, mara tu baada ya mwili kuambukizwa virusi. Matumaini yapo juu kwamba kitakapotumika, huenda kikachukua nafasi ya kipimo cha PCR. Hata hivyo, kipimo hicho kinakabiliwa na vikwazo kidogo vya kutatua kwa upande wa usahihi.

Taarifa hii ni sahihi hadi Julai 2.

52. Mbu wanaweza kueneza virusi vya korona?

Tovuti ya Shirika la Afya Duniani WHO imeelezea wazi kuwa “virusi vipya vya korona haviwezi kuenezwa na mbu.” Inaelezea kuwa hadi leo, kumekuwa hakuna taarifa ama ushahidi unaoashiria kuwa virusi vinaweza kuenezwa na mbu.

Shirika hilo la afya duniani linasema “Virusi vipya vya korona ni virusi vya mfumo wa upumuaji ambavyo vinasambaa hasa kupitia matone madogo yanayotoka pale mtu aliyeathirika anapokohoa ama kupiga chafya, ama kupitia matone madogo ya mate ama mafua yanayotoka puani.”

Shirika hilo linashauri, “Ili kujilinda, safisha mikono yako mara kwa mara kwa kutumia dawa za kuua vijidudu ama safisha kwa maji safi yanayotiririka na sabuni. Pia epuka kuwa karibu na yeyote ambaye anakohoa ama kupiga chafya.”

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni 30 na inapatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK WORLD JAPAN.

49. Nimesikia kwamba mafua ya Kihispania yalitokea katika mawimbi matatu. Tafadhali nisimulie mengi zaidi kuhusiana na mafua hayo.

Janga la mafua la mwaka 1918 linalofahamika pia kama mafua ya Kihispania lilisababishwa na aina mpya ya virusi vya mafua. Shirika la Afya Duniani, WHO linasema takriban watu milioni 500 au takriban robo ya idadi ya watu duniani wakati huo waliambukizwa mafua hayo na milioni 40 kuaga dunia.

Mafua ya Kihispania kwanza yalienea duniani kuanzia msimu wa machipuo wa mwaka 1918 na kupungua wakati wa msimu wa joto. Lakini wimbi la pili la maambukizi lilitokea wakati wa msimu wa pukutizi mwaka huo wa 1918 na kisha wimbi la tatu kujiri mwanzoni mwa mwaka 1919.

Wimbi la pili linaaminika kusababisha vifo vya watu wengi zaidi vikiwa ni vya watu wasiopungua milioni 20 kote duniani.

Nchini Japani, mlipuko wa mafua ya Kihispania ulitokea katika mawimbi matatu kati ya msimu wa pukutizi mwaka 1918 na msimu wa machipuo mwaka 1921. Rekodi zilizohifadhiwa na Wizara ya Mambo ya Ndani wakati huo zinaonyesha kuwa kwa jumla, takriban watu milioni 23.8 waliambukizwa mafua hayo na watu 390,000 kuaga dunia.

Japani ilikumbwa na mlipuko mkubwa wakati wa wimbi la kwanza lililoanza msimu wa pukutizi mwaka 1918 huku watu milioni 21.2 wakiambukizwa mafua hayo na watu 260,000 kufariki. Wimbi la pili lililoanza msimu wa pukutizi mwaka 1919 lilisababisha mlipuko mdogo huku visa milioni 2.4 vya maambukizi vikiripotiwa na watu 130,000 kufariki. Hata hivyo, kiwango cha waliofariki kilikuwa juu zaidi wakati wa wimbi la pili.


Hii leo, wataalam wanaonya kuwa virusi vipya vya korona huenda pia vikawa na wimbi la pili na la tatu sawia tu na mafua ya Kihispania.

Usahihi wa taarifa hii wa kufikia Juni 24 mwaka huu.

48. Ni katika mazingira gani ambapo virusi vipya vya korona huzaliana tena? Je, huzaliana tu vikiwa ndani ya miili yetu?

Tulimuuliza Profesa Kunishima Hiroyuki kutoka Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Marianna ambaye ni mtaalam wa magonjwa ambukizi. Kunishima anasema virusi na bakteria ni baadhi ya vijidudu vidogo sana au vidubini. vinavyosababisha magonjwa.

Bakteria ni viumbehai vya tangu zamani sana vitokanavyo na seli moja. Vinaweza kujizalisha vyenyewe.

Virusi ni vidogo zaidi kuliko bakteria. Vinahusisha jeni au asidi za kiini cha chembe na kufunikwa kwa kiambata cha ulinzi lakini havina seli. Virusi haviwezi kujizalisha vyenyewe. Vinaweza kufanya hivyo tu vikiwa ndani ya seli hai za binadamu au wanyama walioambukizwa.

Hii inamaanisha kuwa virusi vipya vya korona haviwezi kuzaliana kwenye kuta ama sehemu za juu za vitu vinavyovichafua. Lakini tunatambua kuwa virusi hudumisha uwezo wake wa kuambukiza kwenye maeneo kama hayo kwa muda fulani.

Profesa Kunishima anasema kwamba huwa tuna kawaida ya kushika maeneo kama hayo yenye virusi, ikiwemo vitasa vya milango na papi za ngazi, tunapokuwa nje ya makazi yetu. Anasema ili kuzuia maambukizi unapaswa kusafisha mikono yako kwa maji safi yanayotiririka ama kwa kutumia dawa za kuulia vijidudu pale unaporejea nyumbani ama kuwasili ofisini au kabla ya kula.

Taarifa hii ni sahihi kabla ya Juni 24.

47. Unaweza kuambukizwa kwa kubadilishana fedha?

Profesa Mikamo Hiroshige wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Aichi ambaye amebobea katika kudhibiti maambukizi anasema hali inategemea uwingi wa virusi. Anasema lakini ikiwa mtu ana virusi kwenye mikono yake na wakazigusa noti ama sarafu , ni bora kudhani kwamba virusi vitabaki kwenye fedha hizo kwa muda kidogo. Ili kuzuia maambukizi, ni muhimu kuosha mikono yako na sabuni ama dawa ya kuua vijidudu kabla ya kugusa mdomo ama pua yako. Profesa pia anashauri hatua hizi baada ya kugusa chochote ambacho umenunua.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni 23 na inapatikana kwenye tovuti na mitandao ya kijamii ya NHK WORLD JAPAN.

46. Ni kwa muda gani virusi vipya vya korona vinaweza vikaishi kwenye uso wa vitu?

Ripoti moja iliyotayarishwa na watafiti katika Taasisi ya Taifa ya Afya nchini Marekani na mashirika mengine, inasema virusi hivyo kwa kiasi kikubwa hutoweka kutoka kwenye uso wa vitu kadiri muda unavyosonga. Kulingana nao, virusi hivyo havikutambuliwa kwenye shaba nyekundu baada ya saa nne, na wala havikutambuliwa kwenye kadibodi baada ya saa 24.

Hata hivyo, virusi hivyo vilisalia kwenye uso wa plastiki kwa saa 72, na kwenye uso wa chuma cha pua kwa saa 48.

Usahihi wa taarifa hii ni wa kufikia Juni 22.

45. Ni kitu gani kitatokea kwa virusi vitakapogandishwa?

Tulizungumza na Sugawara Erisa, profesa katika Shule ya Uzamili ya Chuo Kikuu cha huduma ya Afya cha Tokyo ambaye amebobea kwenye uzuiaji wa maambukizi.

Wakati kukiwa bado kuna sintofahamu nyingi kuhusiana na tabia za virusi vipya vya korona, tafiti za kimataifa juu ya virusi vya SARS, aina nyingine inayofanana na virusi vya korona, tayari zimefanyika.

Kwa mujibu wa tafiti hizo, wakati virusi vya SARS viliuliwa pale vilipowekwa kwenye mazingira yenye joto kubwa kidogo la nyuzi 56 za selsiasi, kirusi hicho kiliweza kuishi katika nyuzijoto ya chini ya chini ya sifuri ya hasi 80 kwa takribani wiki tatu.

Utafiti huo unaashiria kuwa virusi vipya vya korona huenda vikawa dhaifu dhidi ya joto huku vikiwa na nguvu kidogo katika halijoto ya chini.

Sugawara anasema, ikiwa kwa mfano, virusi vipya vya korona vinapatikana katika sehemu ya juu ya mbogamboga na matunda, vinadhaniwa kuishi katika friji kwa muda mrefu. Hivyo watu wanashauriwa kuua vijidudu nje ya vifaa vya kufungashia kabla ya kuviweka kwenye friji, na kunawa mikono yao vizuri kabla na baada ya kupika. Sugawara anasema bidhaa nyingi zinaweza kuliwa salama ikiwa zitapashwa moto.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni 19.

44. Ikiwa chakula kilichofungashwa kimeathirika na virusi, je, tunaweza kuvitokomeza virusi kwa kukipasha moto chakula hicho kwenye oveni ya mikrowevu?

Oveni za mikrowevu hutumia mawimbi ya sumaku umeme kuzungusha molekuli za maji ndani ya chakula ili kukipasha moto.

Profesa Sugawara Erisa wa Shule ya Uzamili ya Chuo Kikuu cha Huduma ya afya cha Tokyo, mtaalam wa kuzuia maambukizi, anasema chakula chenyewe ni salama kukila ikiwa kimepashwa moto vya kutosha ndani ya oveni ya mikrowevu. Lakini anagusia kuwa hakuna ushahidi kwamba oveni hupasha moto sehemu ya juu ya kifungasho cha chakula kiasi cha kutoka kusababisha virusi kwenye kifungasho hicho kupoteza uwezo wa kuambukiza.

Sugawara anasema ni muhimu kunawa mikono mara kwa mara kabla na baada ya kupika na kula.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni 18.

43. Ni kweli kwamba nchi ambazo zimetumia chanjo ya kifua kikuu ya BCG zina vifo vichache vya virusi vya korona?

Chanjo ya BCG imetengenezwa kutokana na uzao dhaifu wa bakteria wanaosababisha kifua kikuu kwa ng’ombe na ni sawa na bakteria wanaosababisha ugonjwa huo kwa binadamu. Nchini Japani, watoto wote wanapata chanjo hiyo ya kifua kikuu kabla ya kutimiza mwaka mmoja. Sera za chanjo ya BCG zinatofautiana nchi na maeneo. Marekani na Italia ni miongoni mwa nchi zisizo na mpango wa kila mtu wa chanjo ya BCG.

Baadhi ya watafiti nje ya Japani wamedokeza kwamba maeneo yenye utaratibu wa kutoa chanjo ya BCG yana vifo vichache vya virusi vya korona. Majaribio ya kitabibu yanaendelea Australia na Uholanzi kutafiti ikiwa chanjo ya BCG inahusiana na uzuiaji wa maambukizi ya virusi vya korona na kuzuia dalili kuwa kali.

Aprili 3 mwaka huu, Jumuiya ya Japani ya Masuala ya Chanjo iliwasilisha mtazamo wake kuhusiana na suala hilo.

Jumuiya hiyo inasema ufanisi wa chanjo ya BCG dhidi ya virusi vya korona bado haujathibitishwa kisayansi na kwamba kwa wakati huu haipendekezi chanjo hiyo kama njia ya kuzuia virusi hivyo.

Jumuiya hiyo inasema baadhi ya watu wa kizazi cha nyuma kidogo ambao hawakupata chanjo hiyo wanaomba kupatiwa sasa kama ulinzi dhidi ya virusi vya korona. Lakini jumuiya hiyo inasema BCG ni chanjo kwa ajili ya watoto wachanga na usalama na ufanisi wake kwa wazee haujathibitishwa.

Aidha jumuiya hiyo pia inasema kuna haja ya kuepuka ongezeko la matumizi ya BCG nje ya maombi yaliyokusudiwa, ambayo yanaweza kuvuruga usambazaji thabiti wa chanjo hiyo kwa watoto wachanga.

Taarifa hii ni sahihi kufikia Juni 17.

42. “Ni kitu gani kitatokea kwa virusi kwenye ngozi ya binadamu?” na “Je virusi vinakaa kwenye mwili bila ya mtu kuonyesha dalili?”

Tulimuuliza Profesa Kunishima Hiroyuki ambaye amebobea katika magonjwa ya kuambukiza kwenye Shule ya Kitabibu ya Chuo Kikuu cha St. Marianna. Anasema virusi haviwezi kuongezeka isipokuwa vikiingia na kuathiri seli za mnyama aliye hai.

Virusi vya korona vinafahamika hasa kuathiri watu kupitia tando zilizo kwenye pua ama midomo yao na kuzaliana katika seli za koo, mapafu ama maeneo mengine ya wanyama. Virusi haviwezi kuzaliana ikiwa vipo juu ya mkono ama mguu wa mtu.

Lakini ikiwa mtu ana virusi kwenye mikono yake na kisha akagusa macho, pua ama mdomo wake, wanaweza kuathirika. Virusi kwenye ngozi ya mtu vinaweza kuondolewa kwa sabuni, hivyo watu wanapaswa kuwa safi kwa kuosha vizuri mikono yao ama kwa kutumia vitakasa kama vile vya kileo kabla ya kugusa nyuso zao.

Baadhi ya virusi kama vile vinavyosababisha ugonjwa wa malengelenge ya neva ngozini vinabaki kwenye mwili wa binadamu hata baada ya mtu huyo kupona. Lakini kawaida, virusi vya korona ni tofauti, hivyo ikiwa mtu ameambukizwa na kuonyesha dalili, hatimaye, mfumo wa kinga ya mwili wa mtu huyo unafanya kazi na virusi vitatoweka mwilini.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni 15.

41. Je, miali ya urujuani ya jua ama gesi ya ozoni kwa ajili ya kuua bakteria ina ufanisi wa kuua virusi vipya vya korona?

Tulizungumza na Profesa Ohge Hiroki kutoka Chuo Kikuu cha Hiroshima ambaye ni mtaalam wa magonjwa ya kuambukiza. Ohge anasema kuna matarajio kuwa miali mikali ya urujuani kwa muda mrefu maalum dhidi ya virusi na bakteria, ambayo inasababisha magonjwa mengi ni njia yenye ufanisi katika kupunguza uwezo wao wa kuambukiza.

Kuna matarajio kuwa vifaa tayari vinavyotumika ambavyo vinatoa miali mikali ya urujuani vitakuwa vinafaa kukabiliana na virusi vipya vya korona. Kifaa kimoja kinachotumika kwenye hospitali ya Chuo Kikuu cha Hiroshima, katika vyumba vya hospitali vya wagonjwa wa virusi vya korona ambao wameruhusiwa kuondoka, ambapo miali hiyo inatolewa kwenye chumba chote.

Katika hatua nyingine, mwanga wa jua unaaminika kuwa haufai katika kuua virusi kama hivyo ambavyo vinaweza kuangamizwa na vifaa vilivyotajwa awali. Wakati mwanga wa jua ni miali ya urujuani, mwanga huo una miali ya nguvu za aina mbalimbali na haina nguvu kama miali inayotengenezwa na vifaa hivyo.

Kuhusiana na gesi ya ozoni, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa mwezi Mei na kikundi cha watafiti kutoka vyuo vikuu nchini Japani, walibaini kuwa uwezo wa kuambukiza wa virusi vipya vya korona ulipungua baada ya virusi hivyo kuwekwa kwenye gesi ya ozoni kwa takribani saa moja. Ohge anasema gesi ya ozoni iliyotumika kwa ajili ya jaribio hilo ilikuwa na ujazo wa kati ya 1ppm na 6ppm ambayo inadhaniwa kuwa ina madhara kwa binadamu.

Vifaa vinavyotumia gesi ya ozoni kwa ajili ya kuua bakteria na kuondoa harufu ambavyo vinauzwa kwa matumizi ya kawaida, havitumii gesi ya ozoni katika ujazo mkubwa kama huo. Lakini bado haijathibitishwa ikiwa gesi ya ozoni kwenye ujazo mdogo kama huo inafaa katika kupambana na virusi vipya vya korona.

Shirika la Japani la Masuala ya Mlaji linatoa wito kwa watumiaji kuthibitisha na makampuni ya utengenezaji ikiwa wana msingi wa kisayansi wa kudai kuwa bidhaa zao, ikiwa ni pamoja na zile zinazotumia gesi ya ozoni, zinafaa kupambana na virusi vya korona.

40. Je, ni tahadhari zipi zinazopaswa kuchukuliwa wakati unapovaa barakoa wakati wa msimu wa joto?

Ncha ya Kaskazini mwa Dunia inakaribia kushuhudia joto kali la msimu wa joto. Wizara ya Afya, Kazi na Ustawi nchini Japani inasema tahadhari zaidi inapaswa kuchukuliwa ili kuepuka kukumbwa na ugonjwa wa kuzirai unaosababishwa na joto kali mwaka huu, kwani watu wengi wanavaa barakoa kama hatua ya kuepukana na maambukizi ya virusi vya korona.

Wizara hiyo inawashauri watu kuvua barakoa zao ikiwa wamedumisha hali itakikanayo ya kutokaribiana na watu, ambayo inapaswa kuwa mita zisizopungua mbili. Kadhalika wizara hiyo inatoa wito kwa watu kuepukana na kazi za sulubu au kufanya mazoezi wakati wakiwa wamevalia barakoa. Isitoshe, wizara hiyo inawashauri watu kunywa maji mara kwa mara hata ikiwa hawahisi kiu.

Yokobori Shoji ni Profesa wa Shule ya Uzamili ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Nippon aliyetaalamika kuhusiana na masuala ya ugonjwa wa kuzirai unaosababishwa na joto kali. Anasema si lazima kwamba uvaaji wa barakoa unaweza ukamfanya mtu kuwa katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa huo. Lakini anasema uvaaji wa barakoa hufanya iwe vigumu kwa mtu kupumua. Kuna takwimu inayoonyesha kuwa mapigo ya moyo na kiwango cha kupumua viliongezeka kwa asilimia 10, wakati watu walipovalia barakoa. Profesa Yokobori anasema mzigo wa ziada wa kufanya mazoezi au ongezeko la halijoto vinaongeza athari ya kukumbwa na ugonjwa wa kuzirai unaosababishwa na joto kali.

Kulingana na Profesa Yokobori, ni muhimu kuzuia uenezaji wa virusi vya korona kupitia vitone vinavyosalia hewani, lakini wazee au watu wanaoishi peke yao, wanapaswa hasa kutahadhari zaidi inapokuja kwa swala la ugonjwa huo. Wanapokuwa nje, Profesa Yokobori anawashauri watu kuvua barakoa zao na kupumzikia katika maeneo yasiyokuwa na misongamano ya watu, kama vile chini ya mti. Aidha anapendekeza ubadilishaji wa barakoa baada ya kutokwa na jasho, kwani hewa kidogo hupitia kwenye unyevuunyevu wa barakoa.

Taarifa iliyowasilishwa kwenye ripoti hii ni ya hadi kufikia Juni 11.

39. Je, tunapaswa kuwa waangalifu kuhusiana na nini wakati tunapotumia viyoyozi?

Wakati msimu wa joto unapoanza kwenye ncha ya kaskazini mwa dunia, huenda baadhi ya watu wakawa na wasiwasi kuhusiana na upitishaji wa hewa safi katika sehemu ambazo kiyoyozi kinatumiwa kupoesha hewa. Viyoyozi vingi vya kutumiwa nyumbani huzungusha tena hewa iliyo ndani ya nyumba na havitekelezi majukumu ya upitishaji hewa safi. Kuna uwezekano watu wengi hufunga madirisha ya nyumba zao wakati wanapotumia viyoyozi.

Yamamoto Yoshihide ni Profesa mshiriki katika Chuo Kikuu cha Ufundi Anuwai cha Tokyo na pia mwanachama wa Taasisi ya Usanifu Majengo nchini Japani. Nyanja yake ya utaalam inajumuisha upitishaji wa hewa safi kwenye majengo. Profesa Yamamoto anapendekeza kutumiwa kwa pamoja kwa viyoyozi na upitishaji hewa safi.

Katika maeneo yenye misimu minne, Profesa Yamamoto anapendekeza kufunguliwa kwa madirisha ili kwa kiasi fulani kuruhusu hewa safi kutoka nje wakati unapotumia viyoyozi mwanzoni mwa msimu wa joto, wakati joto si kali sana. Wakati chumba chako kinapokuwa na joto kali, poesha hewa hiyo kwa kufunga madirisha kwa muda mfupi au kuyafungua lakini uache nafasi ndogo tu ya kupitisha hewa safi.

Katikati ya msimu wa joto wakati athari ya ugonjwa wa kuzirai unaosababishwa na joto kali inapoongezeka, Profesa Yamamoto anapendekeza kutumiwa mno kwa feni za kuingiza hewa safi kwenye nyumba kama zitumiwazo chooni au jikoni, badala ya kufungua madirisha. Hali sawia pia inapaswa kutumika katika maeneo ya kitropiki.

Makazi mengi yamesanifiwa kupitisha hewa safi kutoka nje wakati feni za kupitisha hewa safi zinapotumika. Hii itaongeza mtiririko wa hewa kati ya ndani na nje ya jengo hata ikiwa madirisha yamefungwa. Tafadhali tafuta ushauri wa wataalam ili kubaini namna upitishaji wa hewa safi unavyofanya kazi nyumbani kwako.

Usahihi wa taarifa hii ni wa kufikia Juni 10.

38. Maswali kutoka kwa wakazi wa kigeni nchini Japani -3-

Swali la kwanza ni “ikiwa nitakumbwa au kushuhudia unyanyapaa unaohusiana na COVID-19, nani ninapaswa kuwasiliana naye?”

Tafadhali wasiliana na kituo cha ushauri cha lugha mbalimbali, cha Yorisoi Hotline, kupitia tovuti yake:
https://www.since2011.net/yorisoi/n2/

Nambari yake ya simu bure ni 0120-279-338.
0120-279-226 kwa mikoa ya Iwate, Miyagi, Fukushima.
Au ukurasa wake wa Facebook ni:
https://www.facebook.com/yorisoi2foreign

Swali la pili ni: “ninanyanyaswa na mwenza wangu, nizungumze na nani kwa usaidizi?”

Waathiriwa wa unyanyasaji wa majumbani wana vyanzo vingi vya msaada, ikiwa pamoja na kutafuta ushauri kwa njia ya simu na mitandao ya kijamii. Pia unaweza kupata huduma ya mtandaoni iliyofasiriwa na taarifa za makazi ya muda.

■Ushauri kupitia mitandao ya kijamii unapatikana kwa saa 24 katika lugha 11. Tafadhali tembelea
https://soudanplus.jp/language .

■Kituo cha Utoaji Ushauri na Usaidizi kwa Dhuluma za Wanandoa
Namba ya simu ni 0570-0-55210 kwa lugha ya Kijapani pekee. Kinakuunganisha na kituo cha ushauri cha jirani nawe.

■Domestic Violence Hotline Plus:
Tafadhali piga 0120-279-889 lakini Kijapani pekee.

Swali la tatu na la mwisho ni: “Nina ujauzito, ninapaswa kuwa na mashaka?”

Wakati ushahidi unaashiria kwamba wajawazito hawapo kwenye hatari kubwa ya kuugua mno kuliko watu wazima wenye afya, maambukizi ya virusi vya korona wakati wa miezi mitatu ya mwishoni ya ujauzito yanaweza kuwa na maendeleo na hali mbaya sawa na wanawake wasio wajawazito. Takwimu zinaonesha Kuwa huhitajiki kuwa na wasiwasi kupindukia kuhusu COVID-19 wakati wa ujauzito. Lakini unapaswa kuendelea kuchukua tahadhari kama vile kuepuka mikusanyiko, kunawa mikono mara kwa mara, na kuzingatia afya yako ya kila siku ya mwili na hisia.

Kwa mengi zaidi, tembelea linki ifuatayo ya lugha mbalimbali:
https://share.or.jp/english/news/for_pregnant_womencovid-19_countermeasures.html

Bonyeza linki ifuatayo kwa kipindi chetu cha runinga cha
Heart Net TV kwa Kijapani rahisi:
https://www.nhk.or.jp/heart-net/article/339

37. Maswali kutoka kwa wakazi wa kigeni nchini Japani -2-

Nchini Japani, raia wa kigeni wanaongezewa muda wa miezi mitatu kutuma maombi ya kupewa viza mpya, kwa ajili ya mabadiliko ya hadhi ya ukazi na kuongezwa muda wa kuishi nchini Japani. Swali la kwanza wanauliza, “Naweza nikaendelea kufanya kazi nchini Japani kwa muda wa nyongeza ya miezi mitatu kuishi nchini Japani hata ikiwa muda wa viza yangu umekamilika?”

Jibu la swali hilo ni “Ndio.” Unaweza ukaendelea kufanya kazi chini ya masharti fulani. Shirika la Huduma za Uhamiaji liliitaarifu NHK World Juni 2 kwamba wakati wa kipindi hiki maalum cha kuongeza muda, una idhini ya kufanya kazi chini ya masharti sawa ya hadhi yako ya ukazi ya awali. Hata hivyo, ikiwa utahitaji kubadilisha masharti yoyote ikiwa ni pamoja na aina ya kazi na mwajiri, ni sharti kwanza utafute ushauri kutoka kwa Shirika la Huduma za Uhamiaji.

Swali linalofuata linauliza, “Je, naweza nikapoteza hadhi yangu ya ukazi ya kufanya kazi au kuwa mwanafunzi nikiwa na kibali cha muda cha kufanya kazi ikiwa siwezi nikafanya kazi au kusoma?”

Jibu la swali hilo ni “Hapana.” Hadhi yako haitafutwa ikiwa umeshindwa kufanya kazi au kusoma kutokana na athari ya virusi vya korona. Lakini ni sharti uthibitishe kuwa umeathiriwa na mojawapo wa mambo yafuatayo:

1. Mwajiri wako au kampuni yako sharti isitishe operesheni zake za kibiashara kwa muda.

2. Unapaswa kuwa umestaafu na unatafuta ajira kupitia mtandaoni, au una kazi unayotarajia kuanza kufanya lakini huwezi ukafika kwenye kampuni husika.

3. Ikiwa taasisi ya elimu ulioandikishwa imefungwa, ikiwa ni pamoja na hali ambapo taasisi ambayo umepangiwa kujiunga nayo imefungwa.

4. Ikiwa taasisi ambayo uliandikishwa itafungwa na haiwezi ikatimiza taratibu zinazohitajika kwa ajili ya wewe kujiunga na taasisi nyingine.

5. Ikiwa kipindi cha kulazwa kwako hospitalini kutokana na ugonjwa vikiwemo virusi vipya vya korona kitakuwa kirefu na kukulazimu kuchukua likizo.

Ikiwa unataka maelezo zaidi, tafadhali itazame tovuti ifuatayo, lakini maelezo yametolewa kwa lugha ya Kijapani pekee, na ikiwa utakuwa na tashwishi kuhusiana na suala lolote unaweza ukathibitisha suala hilo kwa kuwasiliana na Shirika la Huduma za Uhamiaji. Tovuti yenyewe ni http:www.moj.go.jp/content/001319592

Usahihi wa taarifa hii ni wa kufikia hadi Juni 5.

36. Maswali kutoka kwa wakazi wa kigeni nchini Japani -1-

Katika swali la kwanza wanauliza, ‘Nini kinafanyika ikiwa hadhi yangu ya ukazi ya “mgeni wa muda” itamalizika lakini siwezi nikarejea nchini mwangu?’

Katika hali kama hiyo, utaongezewa muda wa siku 90. Ili kupata maelezo ya kina kuhusiana na suala hilo, tafadhali tembelea tovuti ya Wizara ya Sheria ambayo ni:
http://www.moj.go.jp/content/001316293

Katika swali la pili wanauliza, “ikiwa muda wa viza yangu utamalizika kati ya mwezi Machi na Julai mwaka huu, je, muda wake wa matumizi utaongezwa moja kwa moja kwa kipindi kingine cha miezi mitatu?”

Jibu la swali hilo ni la hasha. Lakini raia wa kigeni wanaongezewa muda wa miezi mitatu kwa maombi ya kubadilishiwa upya viza, inapokuja kwa suala la kubadilisha hadhi ya ukazi na kuongezwa kwa muda wa kukaa nchini Japani. Hatua hiyo inalenga kusaidia kupunguza msongamano kwenye vituo vya uhamiaji. Hatua hii ikiwa inafaa tu kwa watu ambao muda wa viza zao unamalizika kati ya mwezi Machi na Julai mwaka huu wa 2020, inatoa nyongeza ya kipindi cha kutuma maombi cha miezi mitatu kutoka tarehe ya kumalizika kwa kipindi cha kuishi nchini Japani. Yaani, ikiwa muda wa kutumika kwa viza yako utamalizika Mei 11, utakuwa na hadi Agosti 11 kutuma maombi ya kuongezewa muda.

Ili kupata taarifa katika lugha mbalimbali, tafadhali tembelea tovuti ya Wizara ya Sheria ya Japani ambayo ni:
http://www.moj.go.jp/content/001316300

Usahihi wa taarifa hii ni wa kufikia hadi Juni 4.

Taratibu za kutuma maombi ya viza hubadilika, hasa wakati huu wa janga la virusi vya korona.
Ikizingatiwa hali zinazomkumba mtu binafsi huwa ni tofauti, tafadhali wasiliana na ofisi ya uhamiaji ikiwa una maswali yoyote.

35. Virusi vya korona vinaweza kuwa hai kwenye halijoto ya hadi kiwango gani, na kupika chakula kunaviua?

Watafiti wanasema virusi vipya vya korona vinaweza kuwa hai kwenye nyuzi joto 37 la selisiasi kwa siku moja lakini joto la nyuzi 56 za selisiasi huua virusi hivyo ndani ya dakika 30. Walibaini virusi hivyo vinakuwa havigunduliki ndani ya dakika 5 kwenye joto la nyuzi 70.

Sugawara Erisa wa Jumuiya ya Kupambana na Kuzuia Maambukizi Japani anasema hamna kisa kilichothibitishwa kuhusiana na kula chakula chenye virusi bila kujali iwapo chakula kilipikwa, na kwamba kupika kwa joto stahiki kutaua virusi hivyo.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni mosi.

30. Je, tunapaswa kufanya nini pale tunaposhindwa kuhisi ladha ya chakula?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka ya hapa Japani, anasema takribani asilimia 30 ya wagonjwa wa virusi vya korona, wamekuwa wakisema kuwa walipatwa na dalili za kushindwa kuhisi ladha au harufu ya chakula.

Kama mtu unapatwa na dalili kama hizo, kuna uwezekano wa kuwa umeathiriwa na virusi hivyo. Lakini dalili kama hizo pia zinaweza kutokea pale unapokuwa umeathiriwa na maradhi mengine. Baada ya dalili hizo kuendelea kwa muda fulani, angalia uwezekano wa kuonana na daktari kama utaendelea kupatwa na homa au kupumua kwa shida.

29. Ni hatari zipi zinaweza kutokana na hatua ya kuwaruhusu watoto kwenda nje kucheza na wenzao wakati huu wa janga la virusi vya korona?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka ya hapa Japani, anasema kuwa baadhi ya shule za msingi na sekondari za chini za hapa Japani, zimefungua tena viwanja vya michezo ili kuwaruhusu watoto kucheza na wenzao wakati huu ambapo shule zimefungwa kwa muda mrefu kote nchini humo.

Anasema wazazi wengi wanaweza kuwa wanajiuliza iwapo hatua hiyo inaweza kusababisha hatari ya maambukizi, japokuwa wanapenda kuwaona watoto wao wakicheza na marafiki zao ili kupunguza msongo wa mawazo unaosababishwa na kukaa ndani kwa siku nyingi.

Sakamoto anasema inaonekana hakuna matatizo makubwa kwa sasa, kama wazazi watazingatia masuala muhimu kama vile kupunguza kadiri iwezekanavyo idadi ya watoto wanaocheza pamoja, na kuhakikisha michezo hiyo inamalizika ndani ya muda mfupi. Pia wanapaswa kuhakikisha watoto wao wananawa mikono yao baada ya kurejea nyumbani.

28. Je, hatari zipi tunakabiliwa nazo tunapokuwa nje tukifanya mazoezi ya kutembea au kukimbia?

Waziri mkuu wa Japani, Abe Shinzo aliusihi umma kujiepusha na shughuli zisizo na umuhimu au zisizo za lazima alipofanya mkutano na wanahabari kutangaza hali ya dharura. Abe pia alisema kuwa sio tatizo kama watu wataenda nje kwa ajili ya mazoezi ya kutembea au kukimbia, jambo ambalo huenda lilitukanganya.

Lakini Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka anasema kuwa hatupaswi kusahau lengo kuu la tangazo hilo, ambalo ni kuwahamasisha watu kujitenga na wengine kwa kiasi fulani. Kama utakimbia wakati unaongea na mtu mwinginge, vijitone vinaweza kusambaa kati ya mtu mmoja na mwingine, jambo ambalo linapaswa kuepukwa.

Lakini ukikimbia nje ukiwa peke yako na hakuna mtu mwingine karibu yako inafaa zaidi kwa sababu hakuna hatari yoyote kubwa inayoweza kutokea.

27. Je, ni namna gani tunaweza kuwa makini, wakati tunaponunua vitu katika maduka makubwa ya manunuzi?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka ya hapa Japani anasema kuwa tunapaswa kukumbuka kusafisha mikono bila kusahau viganja, ncha za vidole na vifundo vya mikono kwa kutumia vitakasa vilivyowekwa nje kabla ya kuingia ndani ya maduka makubwa ya manunuzi. Anaongeza kuwa, ni vyema kwenda kwenye maduka hayo wakati ambao watu wanakuwa sio wengi.

25. Je, ni kwa namna gani tunaweza kuwa makini na kujiepusha na maambukizi ya virusi vya korona kwenye viwanja vya mchezo wa gofu?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema kwamba baadhi ya watu wanaweza kudhani kuwa mchezo wa gofu hauna athari ya maambukizi kwa sababu ni mchezo unaochezwa nje. Lakini uchezaji wa mchezo huo unaojumuisha idadi kubwa ya watu ni hatari sana.

Viwanja vya mchezo wa gofu vyenyewe vipo wazi nje na havipo kwenye maeneo yaliyofungwa.

Lakini kutumia vyumba vya kubadilishia nguo ama kupata mlo kwenye viwanja hivyo kunakohusisha watu wengi kunafanya hatari ya maambukizi kuwa kubwa.

Kando na hilo, tunapaswa kuwa makini juu ya hatari ya maambukizi baada ya kugusa nyuso zetu kwa mikono bila kujua, ilhali mikono hiyo imegusa maeneo yanayoguswa na watu wengi wasiofahamika.

24. Je, natakiwa kufanyaje wakati ambapo wale wanaoishi pamoja kwenye “nyumba ya pamoja ama Share House” wameambukizwa virusi vya korona?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema, katika “Share House” kila mtu ana chumba chake binafsi cha kulala, lakini wapangaji wanatumia jiko na choo kwa pamoja.

Sakamoto anashauri kwamba kitu muhimu cha kufanya ni kuzisafisha sehemu zinazoshikwa mara kwa mara, kama vile mabomba ya maji au swichi za kuwasha taa za umeme kwa kutumia dawa au sabuni zilizozimuliwa, au ikiwa zinapatikana, unaweza ukatumia visafishaji vya kuua viini vya kileo.

23. Je, tunatakiwa kuzingatia mambo gani pale tunapokuwa ndani ya lifti?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema wengi wetu hatuwezi kupanda ngazi kwenda hadi ghorofa ya 10 au ya 20 kwenye majengo. Tunachoweza kufanya ili kuepuka maambukizi ni kutotumia lifti pamoja na watu wengi, na kuepuka kuongea na watu wengine tunapokuwa ndani ya lifti.

Hatua kama hizo zinaweza kupunguza uwezekano wa kuambukizwa.

Sakamoto anaongeza kuwa ni muhimu kutogusa uso wako kwa kutumia kidole ulichotumia kubonyeza vitufe vya lifti.

Baada ya kushika vitufe hivyo, pia ni muhimu kunawa mikono yako kwa maji na sabuni.

22. Je, ukoje ufanisi wa barakoa zinazotumiwa mara moja tu, na zile zilizotengenezwa kwa pamba ambazo zinaweza kufuliwa na kuvaliwa tena?

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema majaribio mbalimbali yamekuwa yakifanyika juu ya ufanisi wa barakoa katika kukabiliana na virusi vya korona.

Majaribio hayo yanaonyesha kuwa barakoa aina yoyote kati ya hizo mbili ina ufanisi kwa kiasi fulani katika kuzuia matone yasitawanyike pale unapokohoa au kupiga chafya.

Sakamoto anasema hata hivyo, ufanisi wa barakoa yoyote kati ya hizo mbili sio timilifu, na kiwango kidogo cha matone kinaweza kupita na kusambaa.

Kwa hiyo ni vyema kujiepusha kwenda nje pale unapokuwa unakohoa au kupiga chafya.

21. Naomba kujua juu ya wagonjwa wa virusi vya korona ambao hawaonyeshi dalili zozote, licha ya kuwa vipimo vinaonyesha kuwa wameambukizwa virusi hivyo.

Mtaalamu wa magonjwa ambukizi Sakamoto Fumie, kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo, anasema kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza wakapona bila ya kuonyesha dalili zozote. Timu ya utafiti nchini China iliripoti kuwa nusu ya wagonjwa waliohojiwa hawakuonyesha dalili kabisa au walikuwa na dalili kidogo.

Lakini Sakamoto anasema tunapaswa kuendelea kufuatilia hali za wagonjwa kwa takribani wiki moja kwa sababu baadhi yao hali zao hubadilika taratibu na wanaweza kuugua kupita kiasi.

20. Je, ninaweza kutumia pombe kali kama vitakasa mbadala?

Wizara ya Afya ya Japani imeamua kuruhusu matumizi ya vinywaji vyenye asilimia kubwa ya kileo vitumike kama mbadala wa vitakasa, ili kufidia usambazaji mdogo uliosababishwa na janga la virusi vya korona. Uamuzi huo unalenga kujibu wito kutoka kwenye taasisi za tiba na vituo vya makazi maalum kwa wazee ambavyo vimekuwa vikihangaika kuweza kupata vitakasa vilivyotengenezwa kwa kileo, yaani alcohol-based sanitizers.

Mwezi Aprili, Wizara ya Afya iliviambia vituo hivyo kuwa vinywaji vyenye asilimia kubwa ya kileo, vilivyotengenezwa na makampuni ya vinywaji vinaweza kutumika kama itakuwa vigumu kupata vitakasa maalum.

Kwa hiyo vinywaji vyenye kileo cha kati ya asilimia 70 na 83 vinaweza kutumika. Baadhi ya aina fulani za vodka zipo kwenye kipengele hiki. Maafisa wa Wizara ya Afya pia wanagusia kuwa vinywaji vyenye asilimia zaidi ya hizo vina uwezo mdogo wa kutakasa, kwa hiyo vinapaswa kuchanganywa na maji.

Maafisa wanasisitiza kuwa hiyo ni hatua ya kipekee kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa vitakasa vyenye kileo, hususan katika vituo vya tiba.

Wanatoa wito kwa umma kuendelea kunawa mikono kwa umakini majumbani ili kuzuia kuenea kwa virusi vya korona.

Data hizi ni za hadi tarehe 27, Aprili mwaka huu.

※Msikilizaji kumbuka kwamba kunywa pombe kali ama vitakasa haikusaidii kuzuia maambukizi ya virusi hivyo bali ni kuhatarisha maisha yako. Idara ya Zimamoto ya Tokyo inatoa tahadhari kuwa vitakasa vya kusafisha mikono vinaweza kuwa chanzo cha moto, basi usitumie karibu na moto kwani vinaweza kulipuka na kuleta madhara makubwa.

16. Kwa kiasi gani dawa ya Avigan inafaa katika kutibu virusi vipya vya korona?

Avigan inayofahamika pia kama Favipiravir, ni dawa ya kutibu influenza iliyotengenezwa na kampuni moja ya kutengeneza dawa nchini Japani miaka sita iliyopita.

Kumekuwa na athari za dawa hiyo zilizoripotiwa kwenye majaribio ya wanyama ya maabara, kwa hivyo serikali ya Japani haijaidhinisha matumizi yake kwa baadhi ya watu kama vile kina mama wajawazito. Dawa hiyo sasa itatumika kuwatibu wagonjwa walioambukizwa virusi vipya vya korona katika visa tu vilivyoidhinishwa na serikali.

Kwa wakati huu, hakuna dawa zingine zinazofahamika zinazofaa kwa matibabu ya wagonjwa wa virusi vipya vya korona, lakini Avigan inatarajiwa kuwa bora katika kutibu virusi hivyo, vinavyozaliana kwa hali sawa na virusi vya influenza. Utafiti juu ya athari za dawa hii unafanyika katika maeneo mengi duniani.

Serikali ya China imetangaza matokeo ya utafiti wa kitabibu uliofanyika kwenye taasisi mbili za tiba. Mojawapo ni iliyopo Mjini Shenhzen kwenye Jimbo la Guangdong ukiwahusisha wagonjwa 80.

Wale ambao hawakutibiwa na dawa ya Avigan walichukua nambari ya katikati ya siku 11 kabla ya matokeo ya majaribio yao kubadilika kutoka kuwa chanya hadi kuwa hasi. Nambari ya katikati ya siku kwa wale waliotibiwa na dawa hiyo ilikuwa nne.

Picha za eksirei zilionyesha kuwa hali ya mapafu ya asilimia 62 ya wagonjwa ambao hawakutibiwa na dawa ya Avigan iliimarika, ilhali asilimia 91 ya wale waliotibiwa na dawa hiyo walipata nafuu.

Serikali ya China imetangaza kwamba matokeo hayo yaliichochea kuijumuisha rasmi dawa ya Avigan kama mojawapo wa dawa za kuwatibu wagonjwa walioambukizwa virusi vipya vya korona.

Nchini Japani, utafiti wa kitabibu unaohusisha wagonjwa 80 wenye dalili zisizokuwa kali ama wale wasioonyesha dalili, umekuwa ukiendelea kwenye taasisi kama vile Chuo Kikuu cha Afya cha Hospitali ya Fujita mkoani Aichi tangu mwezi Machi mwaka huu. Watafiti wanaangazia ni kwa kiasi gani dawa hiyo inaweza ikapunguza wingi wa virusi hivyo.

Kampuni ya Japani inayozalisha dawa ya Avigan imetangaza kwamba imeanzisha majaribio ya kitabibu ili iweze kupata idhini ya serikali. Ikiwa kufaa na usalama wa dawa hiyo vinaweza vikathibitishwa, kampuni hiyo inapanga kutuma ombi la kutaka serikali kuiidhinisha.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Aprili 6.

15. Je, virusi hivyo hujibadili muundo wake wa jeni?

Mwanzoni mwa mwezi Machi, kundi la watafiti la nchini China lilitathmini jeni za virusi vya korona kutoka kwa waathirika zaidi ya 100 wa virusi hivyo kutoka kote duniani. Timu hiyo ya watafiti ilibaini tofauti za kijenetiki walizoziweka kwenye aina mbili za virusi vya korona, aina ‘L’ na ‘S’.

Timu hiyo ilibaini kuwa virusi vya aina ya ‘S’ vina muundo wa jeni unaokaribiana kufanana na ule unaopatikana kwenye popo. Virusi aina ‘L’ vilibainika kwa wagonjwa wengi wa kutoka nchi nyingi za Ulaya na vinaaminika kuwa ni aina mpya kulinganisha na vile vya aina ‘S’.

Profesa Ito Masahiro wa Kitengo cha Sayansi ya Uhai cha Chuo Kikuu cha Ritsumeikan anayetafiti juu ya tabia za virusi, anasema virusi vya korona vinabadilika jeni zake kirahisi na vinaaminika kubadilika kupitia kwa watu wengi wanaoambukizwa na kurejelewa kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Katika hatua nyingine, kuhusu uwezekano wa virusi kubadili jeni zake ili kuweza kuwa rahisi kuambukiza, Ito anasema virusi hivyo bado vipo katika hatua ambayo muundo wake wa kijenitiki haujabadilika kwa kiasi kikubwa. Hata kama kuna tofauti ya jeni kati ya aina ‘S’ na ‘L’, bado kuna uhaba wa taarifa juu ya aina ipi ya virusi inayoweza kusababisha dalili kali. Ito anasema wakati ukali wa ugonjwa na viwango vya vifo vikitofautiana miongoni mwa mataifa, inaaminika kutofautiana huko kunasababishwa na watu wenyewe, ikiwemo tofauti ya uwiano wa idadi ya wazee kwenye nchi husika, tamaduni na utamaduni wa chakula.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Aprili 3.

14. Je, vijana huugua zaidi pale wanapoambukizwa?

Wataalam huwa wanasema kuwa wazee na wale wenye magonjwa yanayosumbua kwa muda mrefu huwa na kawaida ya kuonyesha dalili kali zaidi pale wanapoambukizwa virusi hivyo.

Lakini mwezi Machi, 2020, vyombo vya habari viliripoti kwamba mwanamke mwenye umri wa miaka 21 nchini Uingereza na msichana wa miaka 16 huko Ufaransa, waliokuwa hawana magonjwa mengine, walipoteza maisha baada ya kuambukizwa virusi vipya vya korona.

Visa vya hivi karibuni vinaonyesha kwamba baadhi ya vijana wanaweza pia kusumbuliwa sana na maradhi.

Japani pia imeshuhudia visa vya vijana wakiumwa sana. Kutsuna Satoshi wa Kituo cha Kitaifa cha Afya Duniani na Tiba alisema miongoni mwa wagonjwa zaidi ya 30 aliowatibu, mwanaume mwenye umri wa miaka ya mwanzoni ya 40 ambaye hakuwa na ugonjwa mwingine wa muda mrefu alionyesha dalili kali za maradhi hayo.

Kutsuna anasema mwanaume huyo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya homa na kukohoa tu katika siku kadhaa za mwanzo lakini baada ya juma moja alianza kusumbuliwa sana na homa ya mapafu na alihitaji kifaa cha kumsaidia kupumua kutokana na kuzorota kwa uwezo wake wa kupumua.

Alisema baadaye hali ya mgonjwa huyo iliimarika. Kutsuna alituambia kuwa vijana hawapaswi kudhani kwamba hawawezi kuathirika kwani wao pia wanaweza kuumwa sana.

Shirika la Afya Duniani lilionya kuwa kuna visa vingi vya watu wenye umri wa miaka chini ya 50, kulazwa hospitalini.

Kituo cha Marekani cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa kiliripoti kuwa asilimia 2 hadi 4 ya walioambukizwa wenye umri wa kati ya miaka 20 na 44 wapo kwenye chumba cha wagonjwa walio mahututi.

Taarifa zilizowekwa hapa ni za hadi Aprili mbili.

13. Maambukizi ya virusi vipya vya korona yatasambaa kupitia maji machafu yaliyovuja kutoka kwenye mabomba ya kupitisha maji ya mvua na yale ya maji machafu. Ni kweli?

Virusi vipya na vile vya SARS vyote vinatoka katika familia moja ya korona. Virusi vya korona vilivyosababisha SARS vinajulikana kwa kuzaliana mara nyingi si tu kwenye koo na mapafu bali pia kwenye utumbo.

Pale virusi vya SARS vilipoenea miongoni mwa watu kwenye maeneo mengi duniani mnamo mwaka 2003, maambukizi ya watu wengi yaliripotiwa kwenye majengo yaliyo makazi ya watu huko Hong Kong.

Ilishukiwa kuwa maambukizi ya halaiki yalisababishwa na matone ya maji yenye virusi yaliyovuja kutoka kwenye mabomba yaliyozeeka ya kupitisha maji ya mvua na yale ya maji machafu.

Profesa Kaku Mitsuo wa Chuo Kikuu cha Tiba na Dawa cha Tohoku, mtaalam wa hatua za kuzuia maambukizi, anasema kuwa kuna hatari kidogo ya virusi kuenea kupitia mabomba hayo kwenye nchi zenye kiwango cha juu kiasi cha usafi.

Lakini anasema inawezekana kwa virusi kujipandikiza kwenye vyoo na maeneo ya kukizunguka na unaweza kupatwa na maambukizi kwa kugusa maeneo hayo kwa mikono yako.

Alisema watu wanapaswa kufunika mfuniko wa choo kabla ya kumwaga maji ya kusafisha baada ya kujisaidia na kuhakikisha kuwa wamenawa vema mikono yao baada ya kutoka chooni.

Anasema watu wanapaswa kuhakikisha wanadumisha hali ya usafi kwenye maisha yao ya kila siku, kama vile kwa kusafisha koki za maji, sehemu za kunawia mikono na vitasa.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Aprili Mosi.

11. Je, ukinawa mikono kwa kutumia sabuni, matokeo ni sawa na yale ya kutumia vitakasa vya kileo?

Sakamoto Fumie ni mtaalamu wa udhibiti wa maambukizi kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Mtakatifu Luka jijini Tokyo. Anasema matumizi ya sabuni ni bora kwa kiasi fulani.

Kulingana naye, hii ni kwa sababu sabuni ya kunawia mikono kwa kawaida huwa na kemikali, yaani surfactants zinazoharibu utando wa mafuta unaozingira virusi vya korona. Anasema hii inamaanisha virusi hivyo vinaweza vikaharibiwa kwa kiasi fulani.

Sakamoto anasema vitakasa vya kileo pia ni bora, lakini ikiwa mikono yako ni michafu, wakati mwingine ni vigumu kwa vitakasa hivyo kuingia ndani ya sehemu zilizoambukizwa virusi hivyo.

Sakamoto anawasihi watu kunawa mikono mara kwa mara wakitumia sabuni.

8. Japani imepata dawa bora ya kuzuia au kutibu maambukizi ya virusi vipya vya korona?

Kwa bahati mbaya, hakuna dawa zilizothibitishwa kuwa bora katika kutibu virusi vipya vya korona kama vile dawa za Tamiflu na Xofluza zinazotumiwa kutibu influenza. Kama tu katika mataifa mengine, madaktari nchini Japani wanaangazia kutibu dalili kama vile kumsaidia mgonjwa kupumua kwa kumuwekea gesi ya oksijeni na dripu za kumuongezea maji.

Ingawa dawa bora ya kutibu virusi hivyo bado haijaendelezwa, madaktari nchini Japani na kote duniani wanawatibu wagonjwa wa virusi hivyo kwa kutumia dawa zilizopo za kutibu magonjwa mengine kwa sababu zinaweza zikatumika kutibu virusi hivyo.

Mojawapo wa dawa kama hiyo ni ile ya Avigan, hii ikiwa dawa ya kutibu mafua iliyotengenezwa na kampuni moja ya kutengeneza dawa ya Japani miaka 6 iliyopita. Mamlaka za China zinasema dawa hiyo ni bora katika kutibu virusi vya korona.

Kituo cha Kitaifa cha Japani cha Afya Duniani na Tiba kinasema kilitumia dawa moja ya kupambana na virusi inayotumika kuzuia kuanza kwa ugonjwa wa UKIMWI kwa mgonjwa mmoja aliyeambukiziwa virusi vya korona. Maafisa wa kituo hicho wanasema homa ya mgonjwa huyo ilipungua, na uchovu na tatizo la kupumua kuimarika.

Juhudi za kutafuta dawa ya kutibu virusi vya korona zinaendelea katika nchi kadhaa. Kundi moja la watafiti kutoka kwenye Kituo cha Marekani cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa limeripoti kutumia dawa ya kupambana na virusi inayoendelezwa ili kutibu ugonjwa wa Ebola, kumtibu mwanamume mmoja aliyeugua nimonia kutokana na virusi vipya vya korona. Watafiti wamesema dalili za mwanamume huyo zilianza kuimarika siku moja baada ya kupewa dawa hiyo. Walisema aliondolewa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua kwa kuwekewa gesi ya oksijeni na homa yake kupungua.

Wizara ya Afya nchini Thailand imesema matumizi ya pamoja ya dawa za kutibu mafua na ugonjwa wa UKIMWI ziliboresha hali ya mgonjwa ambaye alipona kutokana na virusi vipya vya korona.

Hata hivyo katika hali zote, wataalam wanasema utafiti zaidi wa kitabibu unahitajika ili kubaini usalama na ubora wa dawa hizo.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Machi 25.

7. Watoto wanaweza wakaonyesha dalili kali ikiwa wataambukizwa virusi vipya vya korona?

Hakuna ripoti yoyote kutoka China kuwa watoto wanaweza wakaonyesha dalili kali ikiwa wataambukizwa virusi vipya vya korona. Tathmini moja iliyofanywa na timu ya wataalam kutoka Kituo cha China cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa iliyohusisha watu 44,672 nchini humo walioambukizwa virusi hivyo kufikia Februari 11 inaonyesha kuwa hakuna mtoto aliye na umri wa miaka 9 au chini ya hapo alifariki kutokana na maambukizi ya virusi hivyo. Ni kifo kimoja tu kilichoripotiwa kati ya wagonjwa walio na umri wa chini ya miaka 20.

Kundi moja la watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Wuhan na taasisi zingine waliripoti kuwa watoto 9 wachanga wenye umri wa kati ya mwezi mmoja na miezi 11 walibainika kuambukizwa virusi hivyo China bara kufikia Februari 6. Wanasema hakuna yeyote aliyezidiwa na ugonjwa.

Profesa Morishima Tsuneo kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Aichi ni mtaalam wa magonjwa ambukizi ya watoto. Profesa Morishima alisema virusi vipya vya korona ni sawia na aina za sasa za virusi vya korona kwa namna fulani na kwamba watoto wanaougua mafua ya kawaida wanaweza wakawa na kiwango fulani cha kinga dhidi ya virusi hivyo.

Hata hivyo Profesa Morishima aliongeza kuwa tunapaswa kuwa na tahadhari kwa sababu maambukizi hayo huonekana kuenea haraka shuleni na kwenye shule za chekechea. Alisema walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wananawa mikono yao ipasavyo na kuhakikisha vyumba wanamoishi vina hewa safi.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Machi 24.

6. Nani ambaye huonyesha dalili kali ikiwa ataambukizwa virusi vya korona?

Shirika la Afya Duniani, WHO linasema vingi vya vifo vilivyosababishwa na virusi hivyo ni vya watu walio na matatizo ya kiafya yanayodhoofisha mfumo wa kinga mwilini ikiwa ni pamoja na shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari na ule wa moyo.

Ili kuwa na uhakika, watu walio na mfumo dhaifu wa kinga za mwili wanapaswa hasa kuwa waangalifu siyo tu dhidi ya virusi vipya vya korona, lakini pia maambukizi ya kawaida kama vile influenza ya msimu.

Wanajumuisha watu walio na matatizo ya kiafya kama vile shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari, ule wa moyo, wale wanaotumia dawa za ushinikizaji wa kinga ya mwili mathalan ili kutibu rumatizimu na wazee.

Watafiti bado hawajabaini jinsi uhatari wa matatizo ya kiafya ya kudumu ya mgonjwa yanavyohusiana na ukali wa dalili zao.

Inapokuja kwa suala la kina mama wajawazito, hakuna takwimu inayoashiria wako kwenye kategoria iliyo kwenye hali hatari ya kuambukizwa virusi vya korona. Lakini kwa ujumla, huwa wanakabiliwa na uwezekano wa kuambukizwa virusi na ikiwa watapata nimonia, kuna uwezekano mkubwa wa wao kukumbwa na dalili kali.

Hakuna takwimu kuhusiana na ni aina gani ya dalili zinazosababishwa na virusi vya korona kwa watoto wachanga. Lakini ikizingatiwa kuwa hawawezi wakachukua hatua za kujilinda kama vile kunawa mikono na kuepukana na sehemu palikofurika watu, walezi wao wanatakiwa kufanya kila wawezalo kuwalinda watoto hao.

5. Ni dalili zipi huonyeshwa na mtu aliyeambukiziwa virusi vipya vya korona?

Kuna ripoti kuhusiana na suala hili iliyochapishwa na timu ya pamoja ya wataalam ikijumuisha wataalam wa Shirika la Afya Duniani, WHO. Timu hiyo ilifanya tathmini ya kina iliyohusu dalili ya watu 55,924 waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya korona nchini China Februari 20 mwaka huu.

Ripoti hiyo inasema asilimia 87.9 ya wagonjwa walikuwa na homa, asilimia 67.7 walikuwa wanakohoa, asilimia 38.1 walilalamikia uchovu, na asilimia 33.4 walikuwa na kikohozi. Dalili zingine zinajumuisha kupungukiwa na pumzi, koo linalowasha na kichwa kuuma. Wale walioambukizwa walianza kuonyesha dalili katika wastani wa siku 5 hadi 6.

Takriban asilimia 80 ya watu walioambukizwa walikuwa kwa kiasi fulani na dalili zisizokuwa kali. Baadhi hawakupatwa na nimonia. Kati ya watu wote walioambukizwa virusi hivyo, asilimia 13.8 walizidiwa mno na ugonjwa na kutatizika kupumua.

Watu wenye umri wa miaka 60 au zaidi na wale waliokuwa na matatizo mengine ya kiafya kama vile shinikizo la juu la damu, ugonjwa wa sukari, matatizo ya moyo, magonjwa ya kudumu ya pumzi na saratani walikuwa na uwezekano mkubwa wa kukumbwa na dalili hatari au zinazoweza zikasababisha maafa. Kuna ripoti chache za watoto kuambukiziwa virusi hivyo au kuzidiwa sana na ugonjwa. Ni asilimia 2.4 pekee ya idadi jumla ya walioambukizwa waliokuwa na umri wa miaka 18 kurudi chini.

Daktari Kutsuna Satoshi wa Kituo cha Kitaifa cha Afya Duniani na Tiba amewatibu wagonjwa waliobainika kuambukizwa virusi vipya vya korona nchini Japani. Daktari Kutsuna alisema wagonjwa aliowaona walikuwa wanatiririkwa na makamasi, walikuwa wanawashwa koo na kukohoa. Alisema wote walikuwa wamechoka na homa ya nyuzi 37 au zaidi iliyodumu kwa karibu wiki moja. Kulingana naye, baadhi yao walipatwa na homa kali baada ya wiki moja, na kwamba dalili huonekana kukaa kwa muda kuliko visa vya mafua ya msimu au magonjwa ambukizi ya virusi na mengine.

Taarifa zilizowasilishwa hapa ni za hadi Machi 19.

4. Tunawezaje tukaua virusi kwenye nguo zetu?

Katika kujibu swali hili, Sugawara Erisa kutoka Chama cha Kuzuia na Kudhibiti Maambukizi nchini Japani anasema hakuna haja ya kutumia vitakasa vyenye vileo. Sugawara anaeleza kuwa virusi vingi huoshwa kutoka kwenye nguo zetu kupitia michakato ya kawaida ya uoshaji nguo, ingawa hili bado halijathibitishwa inapokuja kwa suala la virusi vipya vya korona.

Kuhusiana na bidhaa unazohisi zipo hasa kwenye hatari ya kuambukizwa virusi hivyo kama vile hanchifu iliyotumiwa kufunika mdomo unapokohoa au kupiga chafya, Sugawara anapendekeza uviloweshe kwenye maji yanayochemka kwa kati ya dakika 15 hadi 20.

3. Kina mama wajawazito wanapaswa kujitahadhari na kitu gani?

Huku kukiwa na mlipuko wa virusi vipya vya korona, Chama cha Wakunga na Wanajikolojia cha Magonjwa Ambukizi nchini Japani kilitoa waraka ukiwashauri kina mama wajawazito na wanawake wanaotazamia kuwa wajawazito.

Chama hicho kinasema hadi kufikia sasa, hakujakuwa na taarifa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa wanawake wajawazito kukumbwa na dalili hatari kutokana na virusi vipya vya korona, au kuwepo kwa ripoti za virusi hivyo kusababisha matatizo kwa mtoto ambaye bado hajazaliwa.

Lakini chama hicho kinaonya kuwa kwa ujumla, wanawake wajawazito wanaweza wakawa hatarini ikiwa wataugua nimonia.

Chama hicho kinawashauri wanawake wajawazito kuchukua tahadhari kama vile kunawa mikono ipasavyo kwa kutumia sabuni hasa baada ya kutoka nje na kabla ya maakuli, na kutumia vitakasa mikono vyenye vileo.

Tahadhari zingine zilizopendekezwa zinajumuisha kuepuka kutangamana na watu walio na mafua na wanaokohoa, kuvaa barakoa na kuepuka kugusa pua na mdomo kwa kutumia mikono yako.

Waraka huo ulitayarishwa na Profesa Hayakawa Satoshi wa Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Nihon. Profesa Hayakawa anasema anaelewa wakati kina mama wajawazito wanapokuwa na hofu. Lakini amewataka wanawake kuchukua hatua iliyojikita kwa taarifa sahihi na ya kuaminika kwa sababu aina zote za upotoshaji huenea wakati wa mlipuko wa ugonjwa ambukizi.

2. Ni kwa njia zipi mtu anaweza akaambukizwa virusi hivyo na kujizuia kuambukizwa?

Wataalam wanaamini kuwa virusi vipya vya korona huambukizwa kupitia vitone vya mate au kugusa sehemu iliyo na virusi hivyo kama tu hali inavyokuwa kwa mafua ya msimu au homa. Hii inamaanisha kuwa virusi hivyo huenea kupitia vitone vinavyozalishwa wakati watu walioambukizwa wanapokohoa au kupiga chafya. Mtu pia anaweza akaambukizwa kwa kugusa vitasa vya mlango vilivyo na virusi hivyo, au kanda zinazoning’inia kwenye mabehewa ya treni na kisha kugusa pua au mdomo kwa kutumia mkono uliochafuka. Virusi vya korona vinaaminika kuwa na kiwango sawa cha maambukizi kama mafua ya msimu.

Hatua za msingi za kuzuia maambukizi ya virusi vya korona ni sawa na zile zinazochukuliwa dhidi ya mafua ya msimu. Hizi ni kunawa mikono na kuwa na adabu unapokohoa.

Unaponawa mikono, mtu anashauriwa kutumia sabuni na kuosha kila sehemu ya mikono hadi kwenye kifundo kwa sekunde zisizopungua 20. Au, mtu anaweza akatumia kitakasa mikono chenye kileo. Kuwa na adabu unapokohoa ni njia muhimu ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi. Mtu yeyote yule anashauriwa kufunika pua na mdomo kwa kutumia shashi au kiwiko ili kuzuia kuwanyunyizia watu wengine vitone vilivyo na maambukizi. Njia zingine madhubuti ni kuepuka maeneo yaliyosongamana watu, na wakati unaposalia ndani ya nyumba, kufungua madirisha kila wakati ili kuruhusu hewa safi kuingia kwenye nyumba hiyo.

Nchini Japani, kila kampuni ya treni itaamua ikiwa itafungua madirisha ya mabehewa ya abiria yaliyojaa watu. Watalaam wanasema mabehewa hayo tayari yamewekewa hewa safi kwa kiwango fulani kwa sababu milango ya treni hizo itafunguka wakati zinaposimama kituoni na abiria kuingia au kushuka kwenye treni.

1. Virusi vya korona ni nini hasa?

Virusi vya korona ni virusi wanavyoambukizwa binadamu na wanyama wengine. Kwa ujumla, virusi hivyo huenea miongoni mwa watu na kusababisha dalili sawa na zile za homa kama vile kukohoa, mafua na kutokwa na makamasi. Aina zingine kama vile Ugonjwa wa Mashariki ya Kati Unaoathiri Mfumo wa Upumuaji, almaarufu MERS uliothibitishwa nchini Saudia mwaka 2012, zinaweza zikasababisha nimonia au dalili zingine hatari.

Virusi vya korona ambavyo vimesababisha janga duniani ni vya aina mpya. Watu walioambukizwa hukumbwa na dalili kama vile mafua, vikohozi, uchovu, kupungukiwa na pumzi, koo zinazowasha na vichwa kuuma. Asilimia ya wagonjwa wapatao 80 hupona baada ya kukumbwa na dalili zisizokuwa hatari. Karibu asilimia 20 hukumbwa na dalili hatari kama vile nimonia au hata viungo vingi vya mwili kushindwa kufanya kazi. Watu walio na zaidi ya umri wa miaka 60, au walio na matatizo mengine kama vile kiwango cha juu cha msukumo wa damu, ugonjwa wa kisukari, ule wa moyo, matatizo ya kupumua au saratani wana uwezekano wa kukumbwa na hali hatari au kufariki. Maambukizi machache yameripotiwa miongoni mwa watoto na dalili zao kwa kiasi fulani si hatari.
TOP