Marekani yawawekea vikwazo maafisa wa Iran kufuatia kifo cha mwanamke

Utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden unasema umewawekea vikwazo polisi na maafisa wa usalama wa Iran kutokana na kifo cha mwanamke aliyezuiliwa kwa kuvaa hijabu “isivyofaa.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alitoa taarifa hiyo jana Alhamisi.

Inasema Marekani iliwawekea vikwazo maafisa saba kwa madai ya ukiukaji wa haki za kibinadamu. Adhabu hizo ni pamoja na kushikiliwa kwa mali.

Mahsa Amini aliyekuwa na umri wa miaka 22 alifariki Ijumaa wiki iliyopita baada ya kuwekwa kizuizini mjini Tehran nchini Iran. Kifo chake kimezua maandamano kote nchini humo.

Maandamano yaliendelea jana Alhamisi. Runinga ya serikali ya nchi hiyo iliripoti kuwa watu 17 walifariki katika mapambano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.

Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini humo kinachosimamia masuala ya usalama kilitoa taarifa. Ilisema vikosi hivyo vilitoa wito kwa mamlaka za mahakama kuwatambua na kukabiliana na watu wanaovuruga amani.