Wadau wakuu wakutana kujadili vita nchini Ukraine

Wadau wakuu kwenye mgogoro nchini Ukraine walikutana ana kwa ana jana Alhamisi. Mazungumzo yao yalihusisha wanadiplomasia wa ngazi ya juu waliowakilisha nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ukraine.

Mawaziri wa Mambo ya Nje walikutana siku moja baada ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kuita hadi wanajeshi 300,000 wa akiba, kuchukua hatua ya kutwaa baadhi ya maeneo ya Ukraine na kutishia kutumia silaha za nyuklia.

Mwakilishi wa Marekani ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje Antony Blinken alisema mafuta yameongezwa kwenye moto.

Blinken alisema, “Utaratibu ule wa kimataifa ambao tumekusanyika hapa kuudumisha unavurugwa mbele ya macho yetu. Hatuwezi, hatutamruhusu Rais Putin kuuvuruga.”

Aliongeza kuwa vita vitaisha ikiwa wanajeshi wa Urusi watasitisha tu mapigano.

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov alitetea vita hivyo.

Lavrov alisema, “Tumesema zaidi ya mara moja, tumetoa idadi kubwa ya taarifa za ukweli zinazoonyesha namna Ukraine ilivyojiandaa kutekeleza jukumu la kuipinga Urusi kama hatua ya awali ya matishio dhidi ya usalama wa Urusi.”

Aliondoka mkutanoni punde alipomaliza kuzungumza. Hakumsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dymtro Kuleba akimwambia, “Kamwe hamtashinda.”

Baraza la Usalama halina mpango wa kuidhinisha azimio kwa sababu Urusi, moja ya wanachama watano wa kudumu, inaweza tu kulipigia kura ya turufu. Kuleba aliikosoa Urusi kwa kudumisha haki hiyo.