Maswali yaibuka juu ya athari ya kuingiliwa kati kwa soko la sarafu ya Japani

Maswali yanaibuliwa juu ya ikiwa uingiliaji wa hivi karibuni wa Japani katika soko la ubadilishaji fedha za kigeni utakuwa na athari ya kudumu katika kuimarisha yeni.

Serikali na Benki Kuu ya Japani ziliingilia soko hilo jana Alhamisi kwa kununua yeni na kuuza dola. Ilikuwa hatua ya kwanza ya aina hiyo kufanyika nchini humo tangu mwezi Juni mwaka 1998.

Hatua hiyo ilikuja baada ya sarafu ya Japani kuporomoka kwa muda kwenye biashara ya Tokyo mapema siku hiyo, huku dola ikibadilishwa katika kiwango cha juu cha yeni cha 145. 5.

Kufuatia uingiliaji huo, sarafu ya Japani iliimarika kwa muda huku dola ikishuka kwa zaidi ya yeni 5 hadi kiwango cha chini cha 140. 5.

Tatizo ni kwamba kuna ukomo wa akiba za fedha za kigeni nchini Japani ili kuingilia kati.

Aidha Gavana wa Benki Kuu ya Japani Kuroda Haruhiko anatarajiwa kudumisha sera kubwa ya benki hiyo ya ulegezaji wa fedha, hali inayokinzana na hatua ya hivi karibuni ya Benki Kuu ya Marekani ya kuongeza viwango vya riba.

Wachambuzi wanasema hii inafanya isiwe bayana ni kwa kipindi gani uingiliaji wa hivi karibuni wa Japani na wowote ule wa siku za usoni utaweza kuimarisha yeni.