Kishida atoa wito wa uwekezaji mkubwa zaidi nchini Japani

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio ametoa wito wa uwekezaji mkubwa wa kimataifa kwenye uchumi wa nchi yake na kuahidi uchumi wa ndani kuendelea kukua.

Wito huo ulikuwa sehemu ya hotuba yake kwenye Soko la Hisa la New York jana Alhamisi.

Kishida alitetea sera ya kiuchumi anayoiita “aina mpya ya ubepari.” Alisema imeundwa ili kukuza ukuaji endelevu kwa kutumia “nishati bunifu” ya sekta binafsi na kukabiliana na hatari mbalimbali, kama vile mabadiliko ya tabia nchi.

Aliahidi suala hilo litafanikiwa kwa kutumia “kila mbinu ya sera inayowezekana,” ikiwa ni pamoja na bajeti, kodi na hatua za kulegeza masharti.

Kishida alitaja uwekezaji katika rasilimali watu kuwa moja ya vipaumbele vyake, na akajadili mpango wake wa kufufua soko la ajira.

Aidha alisema mpango huo unahusisha kuweka viwango vya mishahara vinavyozingatia utendaji kazi, badala ya mfumo uliozoeleka unaozingatia uzoefu unaotoa uhakika wa ajira ya kudumu.

Kishida alisisitiza nia yake ya kuhamasisha watu kuwekeza mali zao za kifedha badala ya kuziweka kama akiba. Alitoa wazo la kufuta ukomo wa muda kwenye uwekezaji chini ya mpango wa kutoa misamaha ya kodi kwa wawekezaji binafsi.