Kimbunga cha kitropiki chajikusanya na kukaribia Japani kando ya pwani ya Pasifiki

Maafisa wa hali ya hewa nchini Japani wanasema kimbunga cha kitropiki kimejikusanya juu ya bahari kusini mwa nchi hiyo.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa inasema kimbunga cha kitropiki cha Talas kilikuwa karibu kilomita 300 nje ya mkoa wa Kochi magharibi mwa Japani saa tatu asubuhi kwa saa za nchi hiyo leo Ijumaa.

Kimbunga hicho kinaelekea kaskazini kwa kasi ya kilomita 20 kwa saa. Kinatarajiwa kukaribia magharibi na mashariki mwa nchi hiyo kando ya pwani ya Pasifiki kuanzia leo Ijumaa usiku hadi kesho Jumamosi.

Maafisa wa Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa wanatoa wito kwa watu kwenye njia kitakachopitia kimbunga hicho kutahadhari dhidi ya maporomoko ya ardhi, mito kujaa na mafuriko katika maeneo ya mabondeni, na pia radi na pepo kali.