Watu 6 waripotiwa kuuawa katika maandamano ya hijabu nchini Iran

Raia wa Iran wanaandamana mitaani kupinga kifo cha msichana aliyekamatwa kutokana na namna alivyovaa hijabu yake. Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa watu sita wamefariki katika maandamano hayo.

Vifo hivyo vinajumuisha askari wa vikosi vya usalama aliyeuawa baada ya waandamanaji kukabiliana na polisi wa ghasia na vikosi vya usalama. Wengine wengi wameripotiwa kujeruhiwa.

Mahsa Amini aliyekuwa na umri wa miaka 22 alifariki Ijumaa ya wiki iliyopia akiwa kizuizini jijini Tehran. Ingawa polisi wanasema alifariki kwa mstuko wa moyo, waandamanaji wanaamini alipigwa na polisi.

Nchini Iran, ni lazima wanawake kufunika nywele zao kwa hijabu wakiwa maeneo ya umma. Kwa miezi kadhaa iliyopita, serikali imekuwa ikiongeza ukandamizaji dhidi ya wakiukaji.