UN kuweka uangalizi kwa Putin

Viongozi wa dunia wanapeana zamu kuhutubia katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Jana Jumatano, Rais Volodymyr Zelenskyy aliwapa taarifa kuhusu vita nchini Ukraine. Alimsema Rais wa Urusi Vladimir Putin bila kutaja jina lake.

Zelenskyy alisema. "Kuna mtu mmoja tu miongoni mwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa ambaye anaweza kusema sasa, kama angeweza kukatiza hotuba yangu, kuwa anafurahishwa na vita hivi."

Wajumbe walikuwa wamempa Zelenskyy ruhusa ya kuhutubia mkutano kupitia video. Alisema Urusi inastahili kuadhibiwa kwa uhalifu dhidi ya nchi yake. Aliongeza kuwa inapaswa kupokonywa mamlaka yake ya kura ya turufu katika Baraza la Usalama.

Rais wa Marekani Joe Biden pia alimlenga Putin. Biden alisema, "Mwanachama mmoja wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa amemvamia jirani yake, akijaribu kufuta taifa huru kutoka kwenye ramani. Urusi imekiuka bila aibu kanuni za msingi za Mkataba wa Umoja wa Mataifa,”

Biden alijitaja kama mlinzi wa utaratibu wa kimataifa na Putin kama tishio. Alikuwa amemsikia kiongozi huyo wa Urusi akitishia, katika hotuba yake ya televisheni, kuziweka tayari silaha zake za nyuklia. Alimshutumu Putin kwa "kutowajibika" na "asiyejali."

Biden aliahidi msaada mwingine wa dola bilioni 2.9 za kurejesha usalama wa chakula.