Viongozi wa Japani na Korea Kusini wakubaliana kuendeleza uhusiano wa nchi hizo

Viongozi wa Japani na Korea Kusini wamekubaliana kurekebisha na kuboresha uhusiano wa pande mbili, wakionekana kulitilia maanani suala la kazi wakati wa vita.

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio na Rais wa Korea Kusini Yoon Suk-yeol walikutana pembezoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani kwa karibu nusu saa jana Jumatano kwa saa za hapo.

Walithibitisha umuhimu wa Japani na Korea Kusini pamoja na Marekani kuimarisha ushirikiano wao.

Pia walikubaliana kufanya kazi kwa karibu ili kushughulikia masuala yanayohusiana na Korea Kaskazini. Rais Yoon alisisitiza kuliunga mkono lengo la Japani la kutatua suala la watu waliotekwa nyara.

Walithibitisha kwamba wataamuru uharakishaji wa mabadilishano ya kidiplomasia yanayoendelea, ikiwemo mazungumzo kati ya mawaziri wao wa mambo ya nje, pamoja na kuona wenyewe wanaendelea kuwasiliana kwa karibu.