Waziri Mkuu wa Japani atoa wito wa utekelezaji wa mapema wa CTBT

Waziri Mkuu wa Japani, Kishida Fumio ametoa wito wa uungaji mkono kutoka jumuiya ya kimataifa ili kukomesha majaribio ya nyuklia.

Kishida, ambaye yupo New York kwa ajili ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, alihudhuria mkutano wa ngazi ya viongozi jana Jumatano uliolenga kuruhusu kuanza kwa utekelezaji wa Mkataba wa Kupiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia.

Mkataba huo unalenga kupiga marufuku kabisa milipuko yoyote ya majaribio ya silaha za nyuklia na milipuko mingine.

Umeidhinishwa na mataifa 174, ikijumuisha Japani, lakini bado haujaanza kutumika, kwani nchi zinazomiliki silaha za nyuklia kama vile Marekani na China hazijaidhinisha.

Kishida alisema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umefanya safari ya kuelekea dunia isiyo na silaha za nyuklia kuwa hata ngumu zaidi. Lakini aliongeza bila kujali jinsi safari hiyo ilivyo na milima, kuna haja ya kuendelea.

Kishida alisisitiza umuhimu wa kuimarisha mchakato wa uthibitishaji wa mkataba huo na kuendelea kuhimiza mataifa yasiyotia saini kujiunga na mkataba huo.