BOJ yaendelea na sera ya ulegezaji wa fedha

Benki Kuu ya Japani, BOJ inasema inaendelea na msimamo wake wa ulegezaji fedha kwa kiasi kikubwa, hata kama benki zingine kuu zinapandisha viwango vya riba.

Wajumbe wa bodi ya BOJ walifanya uamuzi huo katika mkutano wa sera wa siku mbili uliomalizika leo Alhamisi.

Benki hiyo itaendelea na kiwango chake cha riba cha muda mfupi katika eneo hasi na kuendelea kununua dhamana za serikali ili kuwa na viwango vya riba vya muda mrefu karibu na asilimia sifuri.

Saa chache tu kabla ya mkutano wa BOJ, Benki Kuu ya Marekani kwa mara nyingine ilipandisha kiwango chake muhimu cha riba kwa robo tatu ya asilimia kwa lengo la kudhibiti hali ya mfumuko wa juu zaidi wa bei nchini humo kuwahi kushuhudiwa katika miongo minne.

Maamuzi ya benki hizo kuu mbili yanaongeza tofauti zaidi ya kiwango cha riba kati ya Japani na Marekani, ambacho kinaweza kuongeza ushukaji wa thamani ya yeni dhidi ya dola. Sarafu hiyo ya Japani imeshuka dhidi ya dola hadi kiwango cha chini zaidi katika kipindi cha miaka 24 huku wawekezaji wanaotafuta faida kubwa nchini Marekani wakisababisha uuzaji wa yeni.