Wizara ya ulinzi ya Japani kusitisha mafunzo kwa maafisa wa jeshi la Myanmar

Wizara ya ulinzi ya Japani imeamua kusitisha kuwapokea maafisa wa jeshi la Myanmar kama wanafunzi kufuatia nchi hiyo kuwaua kisheria watu wanne wakiwemo wanaharakati wanaodai demokrasia.

Wizara hiyo iliwapokea maafisa waandamizi wa jeshi kutoka Myanmar kama wanafunzi, hata baada ya jeshi kuchukua madaraka katika mapinduzi ya mwezi Februari mwaka jana. Lakini mauaji hayo ya mwezi Julai yalipelekea kikundi cha wabunge wa Japani kisichopendelea upande wowote kinachounga mkono mfumo wa demokrasia nchini Myanmar kuitaka Japani kuacha kuwapokea maafisa wa jeshi la nchi hiyo.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Japani Aoki Takeshi aliwaambia wanahabari jana Jumanne kuwa wizara hiyo itaacha kuwapokea wanafunzi hao kuanzia mwaka wa fedha wa 2023 unaoanza mwezi Aprili mwakani.

Aoki alisema wizara hiyo iliamua kuwa haitakuwa sahihi kuendelea na ushirikiano wa kiulinzi na mabadilishano na Myanmar, kama ilivyokuwa kabla ya mauaji yaliyofanyika, kwa kuwa viongozi wa kijeshi wa nchi hiyo walipuuzia maelezo ya Japani ya kuonyesha wasiwasi mkali.