Mashambulizi ya anga katika shule nchini Myanmar yawaua watoto 11

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema watoto wasiopungua 11 wameuawa katika shambulio la helikopta kwenye shule moja kaskazini magharibi mwa Myanmar. Serikali kivuli inayounga mkono demokrasia nchini humo inaamini kuwa shambulio hilo lilitekelezwa na wanajeshi.

UNICEF nchini Myanmar inasema shambulio hilo la anga lilifanyika Ijumaa wiki iliyopita katika maeneo ya kiraia ya Mkoa wa Sagaing. Inasema watoto wasiopungua 15 kutoka shule hiyo hawajulikani walipo. Inalaani shambulio hilo, ikisema shule lazima ziwe salama na watoto wasishambuliwe kamwe.

Serikali hiyo kivuli ya Umoja wa Kitaifa inayounga mkono demokrasia ilisema katika taarifa kwamba askari waliwaweka kizuizini takriban watoto na walimu 20 baada ya shambulio hilo.

Jeshi linasema lilifyatua risasi baada ya kushambuliwa na kundi lenye silaha.

Mtu mmoja ambaye mpwa wake aliuawa alizungumza na NHK.
Alisema, "Sikuona mwili wake. Waliuchukua mara moja. Hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia darasani. Askari walichukua vipande vya maiti na kuviweka kwenye mifuko, na kuvipakia kwenye lori."