Kishida na Truss walaani kura za maoni zilizopangwa na kundi linaloiunga mkono Urusi katika maeneo ya Ukraine

Mawaziri wakuu Kishida Fumio wa Japani na Liz Truss wa Uingereza wamekubaliana kulaani mipango ya kundi linalotaka kujitenga linaloiunga mkono Urusi kufanya kura ya maoni katika baadhi ya maeneo nchini Ukraine.

Kishida na Truss walifanya mazungumzo jana Jumanne jijini New York nchini Marekani kando ya Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Kuhusiana na hali nchini Ukraine, viongozi hao wawili walikubaliana kwamba ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kuungana katika kuendelea kuiwekea vikwazo Urusi na kuisaidia Ukraine. Walikubaliana kwamba mpango wa kundi hilo wa kufanya kura ya maoni kuungana na Urusi haukubaliki.

Kishida na Truss walisema hatua hiyo itazorotesha zaidi uhuru na uadilifu wa maeneo ya Ukraine.

Viongozi hao wa Japani na Uingereza pia walionyesha wasiwasi wao mkubwa kuhusiana na majaribio ya upande mmoja ya kubadili hali ya sasa kwa nguvu katika bahari za China Mashariki na Kusini. China inazidisha uwepo wake kijeshi katika maeneo hayo.