Wanadiplomasia wafutilia mbali kura ‘batili’ za maoni za Urusi

Watu wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi katika maeneo manne ya Ukraine wametangaza kuwa wataitisha kura za maoni kuhusu kujiunga na Urusi. Ukraine ilishutumu hatua hiyo.

Watu hao walisema jana Jumanne kuwa kura zitapigwa kati ya Septemba 23 na 27 huko Donetsk, Kherson, Luhansk na Zaporizhzhia.

Mamlaka za Crimea zilipiga kura kama hiyo mwaka 2014. Kisha vikosi vya Urusi vilivamia na kuitwaa rasi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov alisema, "Tangu mwanzo kabisa wa operesheni maalum ya kijeshi, lakini pia kabla yake, tumekuwa tukisema kwamba watu wa maeneo haya wanapaswa kuamua hatima yao wenyewe."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Dmytro Kuleba alibeza kura hizo kama "batili"." Kuleba alisema, "Warusi wanaweza kufanya chochote wanachotaka. Hazitabadilisha chochote."

Wanadiplomasia, wakiwemo wale kutoka Marekani, wanasema kura hizo ni jibu kwa mafanikio ya Ukraine kwenye uwanja wa vita. Walisema kamwe hawatatambua madai ya kutwaa eneo.