Kishida atoa wito wa kuanza majadiliano juu ya mabadiliko ya Baraza la Usalama la UN

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio ametoa wito wa kuanza majadiliano kuelekea kulifanyia mabadiliko Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Kishida alihutubia Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Jumanne.

Waziri mkuu huyo alisema utaratibu wa kimataifa umetikiswa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambao aliuita kuwa ni kitendo cha kuvuruga ari na misingi ya mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Kishida alisema ni wakati wa kurejea kwenye ari na misingi hiyo. Alisema ni muhimu kufanya mabadiliko kwenye Umoja wa Mataifa na kuimarisha kazi zake hadi mwisho.

Alielezea kuwa uaminifu wa Baraza la Usalama upo mashakani kutokana na uvamizi wa Urusi, ambayo ni mjumbe wa kudumu wa baraza hilo. Alisema mara kadhaa hapo awali, baraza hilo limekuwa likielezewa kama halifanyi kazi na kwamba wakati umefika kuanza majadiliano kuelekea kulifanyia mabadiliko.

Kishida alisisitiza umuhimu wa utawala wa sheria, na kuahidi kwamba Japani itafanya kazi ya kuimarisha baraza hilo ikiwa kama mwanachama wake asiye wa kudumu kuanzia mwezi Januari mwakani.