Hayashi na Park wakubaliana kuendelea na mazungumzo juu ya suala la kazi wakati wa vita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Hayashi Yoshimasa na mwenzake wa Korea Kusini Park Jin walikutana kwa takribani saa moja jijini New York nchini Marekani jana Jumatatu. Hayashi anazuru jiji hilo ili kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Nchini Korea Kusini, hukumu zimetolewa zikiziamrisha kampuni za Kijapani kuwafidia watu wanaosema wao au jamaa zao walilazimishwa kuzifanyia kazi kampuni hizo wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Serikali ya Japani inasema haki yoyote ya madai ilimalizwa kabisa na kikamilifu mwaka 1965, wakati Japani na Korea Kusini ziliporejesha uhusiano.

Hayashi na Park walisema mazungumzo ya kidiplomasia yenye tija yamefanyika. Walithibitisha kuwa wataendelea na mazungumzo ili kutatua suala hilo na kurejesha uhusiano wa pande mbili katika hali nzuri.

Kadhalika walikubaliana kuwa Japani, Korea Kusini na Marekani zitashirikiana kwa karibu katika kukabiliana na Korea Kaskazini ambayo inaongeza kasi ya mipango yake ya nyuklia na makombora.