Kishida aelekea New York kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la UN

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio leo Jumanne aliondoka kuelekea jijini New York nchini Marekani ili kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, baada ya kukawia kwa siku moja kutokana na kimbunga kikali.

Kabla ya kuondoka Uwanja wa Ndege wa Haneda jijini Tokyo, Kishida aliwaambia wanahabari kuwa maudhui ya mdahalo mkuu wa mwaka huu katika mkutano huo yamejikita kwenye mabadiliko muhimu ya kihistoria.

Kishida alisema anataka kuelezea bayana maoni ya Japani kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo namna ya kuimarisha majukumu ya Umoja wa Mataifa wakati msingi wa utaratibu wa kimataifa umetikiswa kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Waziri huyo mkuu amepangiwa kuongoza mkutano wa ngazi ya viongozi unaolenga kutekeleza Mkataba Unaopiga Marufuku Majaribio ya Nyuklia.

Pia anatarajiwa kufanya mikutano tofauti na viongozi wengine akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss.

Kishida alisema angependa kujadili masuala mbalimbali ya dunia na viongozi hao na kusisitiza ushirikiano.

Aliongeza kuwa atatoa hotuba kwenye Soko la Hisa la New York akiangazia sera zake za kiuchumi, ikiwemo “aina mpya ya ubepari.”