Viongozi kutoa hotuba ana kwa ana katika Mkutano wa Baraza Kuu la UN kwa mara ya kwanza baada ya miaka 3

Viongozi wa dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 3 wanajiandaa kutoa hotuba za ana kwa ana katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Wataanza kutoa hotuba hizo leo Jumanne asubuhi katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, UN jijini New York nchini Marekani. Kutokana na janga la virusi vya korona, mkutano huo wa kila mwaka ulifanyika kwa njia ya mtandao mwaka 2020 na mwaka 2021 ulifanyika kwa njia mseto.

Ratiba ya hotuba ilibadilishwa kwa vile baadhi ya viongozi akiwemo Rais wa Marekani Joe Biden walikuwa jijini London kwa ajili ya mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabethi II. Wanatarajiwa kuwasili jijini New York moja kwa moja kutoka London.

Waziri Mkuu wa Japani Kishida Fumio na Marais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Yoon Suk-yeol wa Korea Kusini ni miongoni mwa viongozi waliopangiwa kutoa hotuba siku ya kwanza ya mkutano huo leo Jumanne. Rais wa Marekani Joe Biden amepangiwa kutoa hotuba kesho Jumatano.

Video yenye hotuba iliyorekodiwa awali ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy itaonyeshwa, baada ya pendekezo la kumruhusu afanye hivyo kuidhinishwa na nchi wanachama wa UN.

Pembezoni mwa mkutano huo, Baraza la Usalama linatarajiwa kufanya mkutano wa ngazi ya mawaziri keshokutwa Alhamisi ili kujadili hali nchini Ukraine. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov wanatarajiwa kuhudhuria.