Mfalme wa Japani na Mkewe waelekea nyumbani kutoka Uingereza

Mfalme wa Japani Naruhito na Mkewe Masako wapo njiani kurejea nyumbani wakitokea jijini London, walikohudhuria mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II.

Jana Jumatatu usiku, wanandoa hao walianza safari kutoka Uwanja wa Ndege wa Stansted uliopo viungani mwa jiji la London. Wanatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Haneda jijini Tokyo leo Jumanne jioni.

Wakati wa mazishi huko Westminster Abbey, wanandoa hao walikaa kimya kwa dakika mbili, pamoja na viongozi wengine, ili kumuaga Malkia. Mfalme Naruhito alivaa suti ya asubuhi kwa ajili ya hafla hiyo, wakati Mkewe akivaa gauni rasmi jeusi.

Hatua ya Mfalme Naruhito kuhudhuria mazishi ya Malkia inaakisi uhusiano wa karibu kati ya familia ya kifalme ya Japani na ya Uingereza.

Mfalme Naruhito alikutana na Malkia alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Oxford. Alisoma chuoni hapo kwa miaka miwili katika miaka ya 1980. Wasaidizi wanasema ana kumbukumbu nzuri za mikutano yake na Malkia.