Wafalme na watu wa kawaida wamuaga Malkia Elizabeth II

Viongozi wa dunia na wafalme waliungana na wanachama wa familia ya kifalme ya Uingereza jana Jumatatu kumuaga Malkia Elizabeth. Walimuenzi wakati wa mazishi ya kitaifa kabla ya kuzikwa kwake.

Watu zaidi ya 2,000 walikusanyika katika kanisa la Westminster Abbey jijini London, ambalo Malkia aliolewa na kutawazwa. Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss, Rais wa Marekani Joe Biden na viongozi wengine wa mataifa ya Jumuiya ya Madola walikuwa miongoni mwa waombolezaji.

Mfalme Naruhito wa Japani na Mkewe Masako waliungana na familia za kifalme kutoka kote barani Ulaya kutoa heshima zao.

Umati wa watu ulikusanyika nje kujionea hali ya mambo wakati wasindikizaji wakipita. Walikusanyika mitaani hadi Kasri ya Windsor, makazi aliyoyapenda Malkia wakati wa utawala wake.

Mfalme Charles na wanachama wengine wa familia yake walishiriki ibada iliyojaa taratibu za mpito katika kanisa la St. George. Walitazama wakati jeneza la Malkia likishushwa kwenye kuba ya kifalme kando ya mumewe, Mwana Mfalme Philip.