Idadi ya wazee nchini Japani yaongezeka kufikia rekodi mpya

Leo Jumatatu ni siku ya Kuheshimu Wazee nchini Japani, siku ambayo ni ya mapumziko kitaifa.

Wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo inakadiria kuwa, kufikia Alhamisi iliyopita kulikuwa na rekodi ya watu milioni 36.27 wenye umri wa miaka 65 au zaidi nchini Japani. Hilo ni ongezeko la watu 60,000 kutoka mwaka jana.

Aidha wizara hiyo inasema watu milioni 15.74 kati yao walikuwa wanaume na milioni 20.53 walikuwa wanawake.

Idadi yao ni sawa na asilimia 29.1 ya watu wote nchini Japani, ikiwa ni ongezeko la alama 0.3 kutoka mwaka jana.

Takwimu zilizokusanywa na Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba idadi hiyo ni ya juu zaidi miongoni mwa nchi na maeneo yenye watu zaidi ya 100,000.

Wizara ya mambo ya ndani inasema idadi ya wafanyakazi wazee Japani ilifikia rekodi ya milioni 9.09 mwaka jana.

Uwiano wa wanaofanya kazi wenye umri wa miaka 65 au zaidi katika kundi la wazee ni asilimia 25.1, moja ya idadi kubwa zaidi miongoni mwa nchi kubwa.