Mamlaka ya Mfereji wa Suez kuongeza tozo za usafiri mwakani

Mamlaka nchini Misri zinazosimamia Mfereji wa Suez zinasema zitapandisha tozo za usafiri kwa hadi asilimia 15 kwa meli zinazopita kwenye njia hiyo kuanzia mwaka 2023.

Mamlaka ya Mfereji wa Suez ilitangaza juzi Jumamosi kwamba tozo za usafirishaji kwa meli zinazobeba shehena na meli za kitalii zitaongezeka kwa asilimia 10 huku zile za meli zingine zitapanda kwa asilimia 15 kuanzia Januari mwakani.

Mamlaka hiyo ilitaja kupanda kwa gharama za shughuli za njia hiyo kunatokana na bei ya mafuta kuwa juu.

Kila mwaka, karibu meli 20,000, zikijumuisha meli za kitalii na za makontena, hupita kwenye mfereji huo unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu.

Tozo hizo ziliongezwa mnamo mwaka 2020 na Machi mwaka huu. Kuna wasiwasi kwamba tozo za juu za usafiri zinaweza kuongeza gharama za usafiri na kuongeza kasi ya mfumko wa bei duniani.