Mtu mmoja afariki katika tetemeko la ardhi eneo la Taiwan

Mamlaka ya eneo la Taiwan inasema mtu mmoja amefariki na wengine 142 kujeruhiwa katika tetemeko la ardhi lililotokea jana Jumapili.

Idara ya Hali ya Hewa inasema tetemeko lenye ukubwa wa 6.8 katika kipimo cha Richter lilitokea mashariki mwa Taiwan jana Jumapili mchana na mitetemo mikali ilionekana katika mkoa wa Taitung na mkoa jirani wa Hualien.

Mamlaka ya eneo la Taiwan ilisema kuwa mwanamume mmoja alifariki baada ya kugandamizwa katika kiwanda cha saruji katika mkoa wa Hualien.

Jengo la ghorofa tatu lililokuwa na duka liliporomoka huko Hualien, na kusababisha watu wanne wasiweze kutoka nje na kujeruhiwa, ambao baadaye waliokolewa.

Tetemeko hilo pia lilisababisha sehemu ya treni kuacha njia. Takribani kaya 21,000 kote Taiwan ziliripotiwa kukumbwa na ukosefu wa umeme.

Mashariki mwa Taiwan kumekumbwa na mfululizo wa matetemeko tangu lile la ukubwa wa 6.4 katika kipimo cha Richter kutokea eneo hilo juzi Jumamosi usiku.

Mamlaka za eneo hilo zinatoa wito kwa watu kuwa waangalifu, zikisema tetemeko lenye ukubwa wa 5 katika kipimo cha Richter au zaidi linaweza kutokea katika kipindi cha muda wa wiki moja ijayo au zaidi.