Ukraine yaishutumu Urusi kufanya mashambulizi zaidi kwenye miundombinu ya makazi

Ukraine imevishutumu vikosi vya Urusi kwa kushambulia mara kwa mara miundombinu ya makazi na kusababisha vifo kwa raia wa Ukraine.

Jeshi la Ukraine jana Jumapili lilisema kuwa miundombinu katika maeneo zaidi ya 30 imeharibiwa na mashambulizi ya makombora ya Urusi katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Wizara ya ulinzi ya Uingereza jana Jumapili ilisema Urusi huenda ilipanua shabaha zake “katika jaribio la kudhoofisha moja kwa moja ari ya watu wa Ukraine na serikali.”

Jeshi la Ukraine linaongeza kujibu mashambulizi katika eneo la mashariki na kusini.

Vikosi vya Ukraine vinasema vimekomboa karibu maeneo yote ya mashariki ya Kharkiv kutoka kwenye udhibiti wa Urusi. Vinaaminika kusonga mbele kuelekea eneo la mashariki la Donbas.