Mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II kufanyika leo Jumatatu

Mazishi ya kitaifa ya Malkia wa Uingereza Elizabeth II yatafanyika London leo Jumatatu.

Watu zaidi ya 2,000 kutoka kote ulimwenguni watahudhuria tukio hilo ili kumuenzi malkia huyo aliyetawala kwa muda mrefu zaidi Uingereza.

Malkia alifariki mnamo Septemba 8 akiwa na umri wa miaka 96 katika kasri la Balmoral huko Scotland. Alikaa kwenye kiti cha kifalme kwa miaka 70.

Mazishi yatafanyika Westminster Abbey katikati mwa London kuanzia saa 5 asubuhi, kwa saa za eneo hilo. Yatakuwa mazishi ya kwanza ya kitaifa nchini Uingereza tangu mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani Winston Churchill mwaka 1965.

Mfalme wa Japani Naruhito na mkewe Masako watakuwa miongoni mwa watakaohudhuria.

Vyombo vya habari vya Uingereza vinaripoti kwamba viongozi wa kifalme na viongozi wengine wapatao 500 kutoka karibu nchi na maeneo 200 watahudhuria, akiwemo Rais wa Marekani Joe Biden.

Serikali ya Uingereza imetangaza leo Jumatatu kuwa siku ya mapumziko ya kitaifa.