Kimbunga kikali cha kitropiki cha Nanmadol chaelekea kaskazini mashariki mkoani Yamaguchi

Maafisa wa hali ya hewa nchini Japani wanaendelea kutoa rai kwa watu wa kusini magharibi mwa nchi hiyo kuwa katika tahadhari kubwa kwani kimbunga kikubwa na kikali cha kitropiki Nanmadol kinaelekea kaskazini mashariki juu ya eneo hilo.

Onyo la dharura ya mvua kubwa katika mkoa wa Miyazaki kusini mwa Japani limeshushwa hadi kuwa onyo lakini maafisa bado wanawataka watu kusalia katika tahadhari ya mafuriko na maporomoko ya ardhi.

Kimbunga Nanmadol kilikuwa kinaelekea kaskazini mashariki kwenye mkoa wa Yamaguchi leo Jumatatu, baada ya kulikumba eneo la kusini la Kyushu. Pepo kali zinaathiri karibu eneo lote la Kyushu na sehemu za maeneo jirani ya Chugoku na Shikoku.

Mvua kubwa imekuwa ikinyesha katika eneo kubwa. Mvua za milimita 985 zimerekodiwa katika mji wa Misato mkoani Miyazaki tangu Alhamisi iliyopita. Hiyo ni karibu maradufu ya wastani kwa mwezi wote wa Septemba.

Kimbunga Nanmadol kinatarajiwa kuelekea kaskazini kupitia Kyushu leo Jumatatu na kisha kuelekea mashariki. Baada ya hapo huenda kikaelekea kaskazini mashariki karibu na kisiwa kikuu cha Honshu hadi kesho Jumanne. Mawingu ya mvua yaliyojikusanya jirani na kimbunga hicho yanatarajiwa kusababisha mvua kubwa hasa katika Pwani ya Pasifiki upande wa Magharibi na Mashariki mwa Japani leo Jumatatu.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa inawatahadharisha watu dhidi ya mafuriko katika maeneo ya mabondeni na kufurika kwa mito.