Ndugu za raia wa Japani waliotekwa nyara waitaka serikali kuchukua hatua madhubuti

Ndugu wa raia wa Japani waliotekwa nyara na Korea Kaskazini, wametoa wito kwa serikali ya Japani kuchukua hatua madhubuti kuwarejesha nyumbani wapendwa wao.

Jana Jumamosi, iliadhimishwa mwaka wa 20 wa kufanyika kwa mkutano wa kwanza wa viongozi wakuu wa Japani na Korea Kaskazini, ambapo Korea Kaskazini ilikiri kufanya vitendo hivyo. Watu watano waliotekwa nyara walirejeshwa nchini Japani baada ya mkutano huo.

Hata hivyo, 12 kati ya 17 waliotekwa nyara wanaotambuliwa rasmi na serikali ya Japani, bado hawajulikani walipo.

Wazazi wanane wa waliotekwa nyara wamekwishafariki dunia bila ya kutimiza azma zao za kuungana na watoto wao.

Katika maandamano jana Jumamosi huko mjini Saitama, kaskazini mwa Tokyo, mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 45 wa Taguchi Yaeko aliyetekwa nyara, alisema kuna kesi nyingi kama hizo.

Iizuka Koichiro alisema anataka serikali ielewe juu ya hali isiyokuwa ya kawaida katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili. Aliusihi utawala wa Waziri Mkuu Kishida Fumio kuangazia mitazamo mipya ili kuondoa mkwamo na kuwarejesha nyumbani waliotekwa.