Waombolezaji wengi zaidi wajitokeza kumuaga Malkia Elizabeth mwishoni mwa juma

Waombolezaji wanaendelea kukusanyika kwenye Ukumbi wa Westminster kutoa heshima zao za mwisho kumuaga Malkia Elizabeth wa Pili.

Kwa wakati fulani jana Jumamosi, serikali ya Uingereza ilionya kwamba muda wa kusubiri kwenye foleni ungeweza kuwa hata saa 24.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo pia viliripoti foleni ya kusubiri kumuaga Malkia inaweza kufikia umbali wa kilomita 16, na kuonya kwamba wahudhuriaji hawataweza kukaa chini na kupumzika kwani foleni hiyo inapaswa kuendelea kusogea.

Huduma za Dharura ya London ilisema wahudumu wa afya waliwahudumia watu 435 waliokuwa kwenye foleni Jumatano na Alhamisi wiki hii, na kwamba 42 kati yao walipelekwa hospitalini.

Watu waliopo mwishoni mwa foleni hiyo walisema wapo radhi kusubiri kwa kadiri iwezekanavyo, huku baadhi yao wakisema wamebeba chakula ili kuweka kambi kwa usiku kucha.

Ukumbi wa Westminster unawapokea waombolezaji hadi saa 12:30 Asubuhi siku ya Jumatatu, ambayo ni siku ya mazishi ya kitaifa.