Baadhi warejea Kharkiv baada ya Ukraine kujibu mapigo

Wakazi wanarejea taratibu katika baadhi ya maeneo ya eneo la mashariki mwa Ukraine la Kharkiv. Hatua hiyo inakuja wakati Ukraine ikifanya mashambulizi ya kujibu mapigo katika eneo hilo.

Kharkiv imekuwa katika mapigano makali tangu Urusi ilipoanza uvamizi.

Maeneo ya mashariki mwa mji wa Kharkiv yameshambuliwa zaidi. Majengo katika maeneo hayo yameharibiwa na magari yaliyochomwa moto yanaweza kuonekana kando ya barabara.

Wanajeshi wa Urusi bado wanafanya mashambulizi katika eneo hilo. Lakini mashambulizi yamepungua tangu vikosi vya Ukraine vilipoanzisha mashambulzi ya kujibu mapigo mapema mwezi huu. Vikosi hivyo viliyachukua tena maeneo mengi ya eneo hilo.

Maduka mengi katika mji huo bado yamefungwa, lakini migahawa michache imefunguliwa tena.

Kwa upande mwingine, Rais Vladimir Putin wa Urusi aliwaambia waandishi wa habari juzi Ijumaa kuwa mashambulizi ya kujibu mapigo ya jeshi la Ukraine hayatabadili mipango ya Urusi.