UN yapiga kura kumruhusu Zelenskyy kuhutubia Mkutano Mkuu kwa njia ya video

Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa umepiga kura jana Ijumaa ya kuruhusu hotuba iliyorekodiwa kwa njia ya video ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy kuonyeshwa wiki ijayo pale viongozi wa dunia watakapokusanyika jijini New York nchini Marekani.

Serikali ya Ukraine iliomba kwamba Zelenskyy aruhusiwe kuhutubia mkutano huo kwa njia ya mtandao. Ilisema uvamizi unaoendelea wa Urusi umefanya kuwa vigumu kwa kiongozi huyo kusafiri salama kwenda na kurudi kutoka makao makuu ya UN.

Ombi hilo liliidhinishwa na nchi wanachama 101 wa UN. Walilaani uvamizi wa Urusi na kusema hali inathibitisha ruhusa hiyo.

Kwa upande mwingine, Urusi, Belarus, Korea Kaskazini na nchi zingine nne zilipiga kura ya kupinga ombi hilo. China, Brazil na mataifa mengine 17 yalijizuia kupiga kura hiyo. Yalisema haikuwa sawa kuipatia Ukraine ruhusa hiyo ya kipekee.