Kimbunga Nanmadol chakaribia kusini magharibi mwa Japani

Maafisa wa hali ya hewa wametoa tahadhari ya upepo mkali, mawimbi makubwa na kimbunga kwa Mkoa wa Kagoshima uliopo kusini magharibi mwa Japani. Maafisa hao wanasema kimbunga kikali kinaweza kusababisha aina ya majanga ambayo huonekana mara moja tu katika miongo michache.

Leo Jumapili asubuhi jicho la Kimbunga Nanmadol lipo kusini mwa Kyushu. Na kimbunga hicho kinasogea taratibu kuelekea kaskazini-kaskazini-magharibi. Kinatarajiwa kusogea karibu na Kyushu ama kinaweza kuwa kimefika hadi kesho Jumatatu.

Maafisa hao wanasema kiwango cha juu cha upepo wa hadi kilomita 180 kwa saa kitalikumba eneo la kaskazini na kusini mwa Kyushu pamoja na Visiwa vya Amami kikiwa na dhoruba inayofikia kilomita 252 kwa saa leo Jumapili.

Kyushu kusini inaweza kupata mvua za hadi milimita 600 katika kipindi cha saa 24 hadi kesho Jumatatu asubuhi.

Pia mamlaka ya hali ya hewa inatoa onyo kwamba wakati kimbunga kikiendelea kuwa kikubwa, mvua na upepo vinaweza kuongezeka hata katika maeneo ya mbali na kimbunga hicho. Mvua mkubwa unatarajiwa katika eneo la magharibi na baadhi ya maeneo ya mashariki mwa Japani hadi kesho Jumatatu. Kimbunga hicho kinatabiriwa kuelekea kaskazini mashariki na kusafiri katika kisiwa kikuu cha Japani cha Honshu hadi kesho kutwa Jumanne.