Mkuu wa UN apiga kengele ya amani, arejelea wito wa amani

Hafla ya kila mwaka ya upigaji Kengele ya Amani imefanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York nchini Marekani. Akihutubia kwenye hafla hiyo Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema dunia inapaswa kushirikiana kukabiliana na changamoto zinazoshabihiana, badala ya kupigana.

Hafla hiyo ilifanyika jana Ijumaa kwenye bustani ya Japani, ikiwa ni kabla ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani itakayoadhimishwa Septemba 21.

Japani ilitoa kengele hiyo mwaka 1954 chini ya mkakati wa ‘Nakagawa Chiyoji’, mwanaharakati wa amani kutoka mkoani Ehime, magharibi mwa Japani. Kengele hiyo iliundwa kutokana na sarafu zilizotolewa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Binti wa Nakagawa aitwaye, Takase Seiko, ni miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, aliwaambia wahudhuriaji kuwa, “Tunapokutana leo, amani inashambuliwa,” akionekana kurejelea uvamizi wa kijeshi wa Urusi nchini Ukraine.

Aliongeza kusema, “Badala ya kupigana kwenye uwanja wa vita, tunapaswa kushirikiana kutatua changamoto zinazotukabili, kama vile umasikini, njaa, kukosekana kwa usawa, mabadiliko ya tabia nchi na kuangamia kwa viumbe anuai.