Kimbunga Nanmadol chakaribia Okinawa, kusini mwa Kyushu

Maafisa wa hali ya hewa nchini Japani wamesema kimbunga kikali na kikubwa kiitwacho Nanmadol kinatarajiwa kufika maeneo ya Visiwa vya Daito Mkoani Okinawa leo Jumamosi, na eneo la Amami Mkoani Kagoshima na kusini mwa eneo la Kyushu kufikia Jumamosi usiku.

Baada ya kupita eneo la Kyushu Jumatatu ijayo, Kimbunga Nanmadol kinatabiriwa kuelekea kaskazini mashariki na kupita kwenye kisiwa kikuu cha Japani cha Honshu, kuelekea mashariki na kaskazini mwa Japani hadi Jumanne ijayo.

Kiwango cha mvua kwa kipindi cha saa 24 hadi baadae leo Jumamosi mchana, huenda kikafikia milimita 250 huko kusini mwa Kyushu, Amami na Tokai.

Maafisa wa hali ya hewa wanatoa wito kwa wakazi wa maeneo husika kuangazia mara kwa mara utabiri wa hali ya hewa na tahadhari, kujiepusha na safari zisizo muhimu, na kujiandaa.