Mfalme Charles ziarani Uingereza kabla ya maziko ya Malkia Elizabeth

Mfalme Charles amekuwa kwenye pilika nyingi akisafiri kote nchini Uingereza kuhudhuria ibada za kumbukumbu kabla ya maziko ya Malkia Elizabeth. Alihitimisha ziara yake kwa kutembelea Wales jana Ijumaa.

Kwa kipindi cha miongo sita, Charles alikuwa ni Mwana Mfalme wa Wales. Akiwa na mkewe Camilla, walilakiwa na hadhira kubwa walipokuwa wakipita kuelekea kwenye Kanisa Kuu la Llandaff.

Baadae walitembelea Bunge la Wales. Mfalme Charles alisema “anashukuru sana” kwa fursa ya kuwatumikia watu wa Wales akiwa ni Mwana Mfalme.

Jijini London, msururu wa waombolezaji wanaosubiri kutoa heshima zao za mwisho kuuaga mwili wa Malkia, uliendelea kuwa mrefu. Miongoni mwao alikuwa ni David Beckham, nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya soka ya Uingereza.

Alisema kuwa angependa kujumuika na watu wengine wote kwenye shughuli hizo za kutafakari maisha ya Malkia pamoja na kumbukumbu aliyoiacha duniani.

Maandalizi ya mazishi ya Malkia Elizabeth yanayotarajiwa kufanyika Jumatatu ijayo sasa yapo kwenye hatua za mwisho.