Putin atumai kupanuliwa kwa Shirika la Ushirikiano wa Shanghai kuzikabili nchi za Magharibi

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amesisitiza juu ya kile anachoona kuwa ni hitaji la kulipanua Shirika la Ushirikiano wa Shanghai, SCO, kama njia ya kukabiliana na nchi za Magharibi. SCO ni mpango-mkakati wa kimaeneo unaoongozwa na China na Urusi.

Putin alihudhuria mkutano wa viongozi wakuu wa SCO huko Samarkand nchini Uzbekistan jana Ijumaa. Rais Xi Jinping wa China na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi walikuwa ni miongoni mwa waliohudhuria.

Mkutano wa mwaka huu uliwakutanisha viongozi hao wakuu ana kwa ana kwa mara ya kwanza tangu mlipuko wa virusi vya korona ulipoanza.

Putin alibainisha kwamba SCO ni mpango-mkakati mkubwa zaidi wa kimaeneo duniani, na kudai kwamba jukumu lake limeongezeka katika juhudi za kutatua changamoto za kimataifa.

Kwa upande wake Rais wa China, Xi Jinping, aliahidi kuchochea maendeleo ya SCO na kuhakikisha usalama wa Asia, Bara la Ulaya na dunia kwa ujumla, huku akihakikisha amani an ustawi.