Ndugu wa mateka wa Japani warejelea wito wa kupatikana suluhu

Ndugu wa raia wa Japani waliotekwa nyara na Korea Kaskazini miongo kadhaa iliyopita, wamerejelea wito wao wa kutaka kurejeshwa kwa wapendwa wao. Ndugu hao walikutana usiku wa kuamkia siku ya maadhimisho ya mwaka wa ishirini tangu kufanyika kwa mkutano wa viongozi wakuu wa Japani na Korea Kaskazini, ambapo Korea Kaskazini ilikiri juu ya utekaji nyara huo.

Kufuatia mkutano huo uliofanyika Septemba 17 mwaka 2002, mateka watano walirejeshwa nchini Japani. Hata hivyo, mateka 12 kati ya 17 wanaotambuliwa rasmi na serikali ya Japani, bado hawajulikani walipo.

Wakati kukiwa na mkwamo kwenye mazungumzo baina ya pande hizo mbili, baadhi ya ndugu wa mateka hao tayari wamefariki dunia.

Yokota Takuya, kaka mdogo wa Megumi na kiongozi wa sasa wa kundi hilo, alisema katika mkutano huo jijini Tokyo jana Ijumaa, kwamba baadhi ya wawakilishi wa kundi hilo waliokutana na waandishi wa habari baada ya mkutano wa kihistoria wa viongozi wakuu wa nchi hizo uliofanyika miaka 20 iliyopita, hawapo tena duniani. Alizisihi serikali za nchi zote mbili kutambua kwamba hakutakuwa na suluhu ya tatizo hilo hadi pale mateka hao watakaporejea na kuungana na wazazi wao wakiwa hai.