Kimbunga ‘chenye nguvu’ cha Nanmadol chakaribia eneo la Okinawa na Amami

Maafisa wa hali ya hewa wa Japani wanasema kimbunga kikubwa na chenye nguvu cha Nanmadol kinatarajia kupita karibu na Mkoa wa Okinawa na eneo la Amami katika Mkoa wa Kagoshima kufikia kesho Jumamosi. Huenda kikafika eneo la Kyushu keshokutwa Jumapili.

Maafisa wa Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa wanasema kuwa kimbunga hicho ni hatari na wanawaasa wakazi kuchukua tahadhari kubwa dhidi ya uwezekano wa majanga yatakayosababishwa na upepo mkali na mvua kubwa.

Maeneo ya Okinawa na Amami yanatabiriwa kuwa na upepo mkali. Katika eneo la Amami, upepo wa hadi kilomita 108 kwa saa unatarajiwa kutokea hadi kesho Jumamosi.

Bahari pia zitakuwa na mawimbi makubwa karibu na Kyushu kusini, Okinawa na Amami, huku mawimbi ya urefu wa mita 10 yakitarajiwa kesho Jumamosi.

Maafisa wa hali ya hewa wanatoa wito wa kuchukua tahadhari dhidi ya dhoruba, na mawimbi makubwa, pamoja na maporomoko ya ardhi, mafuriko na mito kujaa.